Vyombo vya habari ni nguzo ya kulinda wahamiaji wa kazi- ILO

WhatsApp-Image-2026-06-10-at-07.02.41-1024x683 Vyombo vya habari ni nguzo ya kulinda wahamiaji wa kazi- ILO

Na Mary Geofrey, Dar es Salaam

VYOMBO vya habari vimetajwa kuwa nguzo muhimu katika kulinda haki na heshima ya wahamiaji wa kazi nchini Tanzania na Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki, huku wadau wakisisitiza uandishi wa habari wa uchunguzi na uwajibikaji.

Mshauri Mkuu wa Kiufundi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Aida Awel, amesema hayo jana Juni 10 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao maalum kilichoandaliwa na ILO kwa lengo la kujadili masuala ya wahamiaji wafanyakazi nchini Tanzania na waliopo katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kikao hicho kimejumuisha wadau wa serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi na wanahabari waliojadili namna uhamiaji wa kazi unavyobeba simulizi za kibinadamu na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Awel amesema: “Kila takwimu ya uhamiaji ina simulizi ya kibinadamu. Hawa ni vijana wanaotafuta ajira ya kwanza, wazazi wanaosaidia familia zao na wafanyakazi wanaotafuta heshima na maisha bora.”

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Oddo Hekela, anahimiza waandishi wa habari kutumia istilahi sahihi na kuepuka neno “wahamiaji haramu,” akisema: “Lugha tunayotumia ina maana kubwa. Tuwataje kama wahamiaji wasio wa kawaida.”

Naye Mkurugenzi wa Jinsia, Wanawake na Vijana wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Mratibu wa Kituo cha Rasilimali kwa Wafanyakazi Wahamiaji, Nasra Shargy, ameonya kuwa njia zisizo salama huwafanya wahamiaji kukumbwa na unyonyaji na biashara haramu ya binadamu, akisisitiza jukumu la vyombo vya habari katika kuibua maovu ya ajira.

Amebainisha kuwa uhamiaji unaweza kuleta fursa kwa wafanyakazi na kuchangia ukuaji wa uchumi unaposimamiwa vizuri.

“Lakini kuwa njia zisizo salama za uhamiaji huwaweka wafanyakazi kwenye hatari ya unyonyaji, matumizi mabaya, biashara ya binadamu na ukiukwaji wa haki za kazi,” amesisitiza.

Mkuu wa Utafiti na Uhamasishaji Sera katika Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Renatus Mbamilo, ameongeza kuwa uhamiaji wa kazi ni suala tata linalohitaji uandishi wa habari wa kina na wa ushahidi, akihimiza wanahabari kuchunguza vyanzo mbalimbali na kuangazia uhamiaji wa ndani na nje.

Wadau hao wamesisitiza kuwa uhamiaji si tatizo, bali tatizo ni pale unapotokea kwa njia zisizo salama na zisizo na heshima kwa wafanyakazi.

Mkutano huo ulimalizika kwa wito wa ushirikiano thabiti kati ya serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi, washirika wa maendeleo na vyombo vya habari ili kuimarisha mifumo ya uhamiaji wa kazi kwa usalama na heshima ya wafanyakazi.

WhatsApp-Image-2026-06-10-at-07.02.40-1-1024x683 Vyombo vya habari ni nguzo ya kulinda wahamiaji wa kazi- ILO
WhatsApp-Image-2026-06-10-at-07.02.40-1024x683 Vyombo vya habari ni nguzo ya kulinda wahamiaji wa kazi- ILO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *