Rais Samia kuhitimisha miaka 60 ya JKT Dodoma

Na Sarah Moses.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa(JKT) Julai 10,2023 jijini hapa.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 08,2023 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema kuwa anawaalika Viongozi wote wa Serikali, Taasisi mbalimbali,watumishi na wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria siku ya kilele cha maadhimisho hayo.

Amesema katika kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na Gwaride la Vjana wa JKT,maonesho ya vifaa mbalimbali vya SUMAJKT na burudani za ngoma kutoka vikundi vya JKT na wasanii mbalimbali.

Nawakaribisha wananchi wote wajitokeze kuhudhuria siku ya Jumatatu kuanzia saa 12:30 asubuhi katika uwanja wa Jamhuri wa Dodoma.

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa jitihada anazozifanya na kuhakikisha JKT linaendelea kuwa kitovu cha malezi bora kwa vijana wa kitanzania” amesema Waziri Bashungwa

Aidha Waziri huyo amesema kuwa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JKT kimetanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na JKT Marathon 2023 iliyofanyika June 25 jijini Dodoma.

“Hii ni marathon ya kwanza kuandaliwa na JKT tangu kuanzishwa kwakwe na ilifana sana” amesema.

Lakini pia Makamu wa Rais DK. Philip Mpango mnamo julai 1 ,2023 alifanya uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu makao makuu ya JKT yaliyopo Chamwino Dodoma na kufungua maonesho ya bidhaa siku hiyo hiyo ambayo yanaendelea mpaka sasa katika viwanja vya Medeli East mkabala na SUMAJKT House.

Hata hivyo Waziri Bashungwa amesema kuwa pia walifanya shughuli za kijamii kama kutembelea hospitali ya Uhuru iliyopo wilaya ya Chamwino pamoja na vituo vya kulelea watoto wenye uhitaji .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *