Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imesema imekamilisha zoezi la kuwatambua na kuandaa utaratibu wa kuingiza katika daftari la pensheni wazee waliopigana Vita ya Kagera, hatua inayolenga kuwatambua rasmi na kuwahudumia kwa heshima stahiki kutokana na mchango wao katika ulinzi wa nchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, wakati akihitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma, leo Jumanne Mei 19, 2026.
Waziri Dkt. Nyansaho amesema wazee walioshiriki Vita ya Kagera walikuwa katika makundi matatu, ikiwemo wanajeshi waliokuwa Jeshini wakati wa vita, wananchi waliojitolea kupigania nchi pamoja na Jeshi la Akiba (mgambo) lililoshiriki katika ulinzi wa taifa katika kipindi hicho.
Amefafanua kuwa baada ya kumalizika kwa vita hiyo, baadhi ya watu hao walipata nafasi katika vyombo vya ulinzi na usalama, huku wengine wakikosa sifa za ajira kwa wakati huo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo majeraha waliyoyapata katika uwanja wa mapambano.
Dkt. Nyansaho amesema katika kipindi hicho, Serikali kupitia uongozi wa wakati huo ilitoa kiasi cha shilingi 5,000, malipo yaliyofahamika kama “Ahsante Nyerere” kwa baadhi ya waliokuwa wapiganaji, hatua iliyolenga kuonyesha shukrani kwa mchango wao.
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, alitoa maagizo Wizara ya Ulinzi kufanya tathmini na kuhakikisha wazee hao wanatambuliwa rasmi na kuingizwa katika mfumo wa pensheni kama sehemu ya kuenzi mchango wao kwa taifa.
Waziri huyo amesema kazi ya kuwatambua wazee hao imekamilika, ambapo jumla ya zaidi ya wazee 7,800 wametambuliwa kupitia watendaji wa Jeshi la Akiba katika ngazi ya wilaya pamoja na ofisi za Wakuu wa Wilaya.
Ameeleza kuwa majina ya wazee hao tayari yamewasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya uhakiki, hatua itakayowezesha kuanza kwa mchakato wa kuwalipa pensheni kama ilivyoagizwa na Serikali.
