Rais Samia apongezwa kwa jitihada zake za kulinda amani na utulivu wa nchi

jafo-1024x682 Rais Samia apongezwa kwa jitihada zake za kulinda amani na utulivu wa nchi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe, Selemani Jafo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, ulinzi na usalama.

Dkt. Jafo ametoa pongezi hizo leo Jumanne Mei 19, 2026 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma.

Amesema Rais Samia amejiapambanua kwa namna anavyoendelea kuweka nguvu katika kuhakikisha wizara hiyo inafanya kazi zake kwa ufanisi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amempongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho kwa kazi kubwa aliyoanza kuifanya ndani ya muda mfupi tangu alipopewa dhamana hiyo, akisema ameonyesha uongozi wenye hekima pamoja na kushirikiana vizuri na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Faraji Mnyepe.

Dkt. Jafo pia amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jacob Mkunda kwa kazi kubwa ya kusimamia jeshi hilo, akieleza kuwa Watanzania wana imani na heshima kubwa kwa jeshi lao.

Amesema Tanzania inaendelea kuheshimika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kutokana na uimara wa jeshi lake ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kusimamia amani na kutatua migogoro katika bara la Afrika na maeneo mbalimbali duniani.

Mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa kuiwezesha wizara hiyo ili iweze kuendelea kusimamia kikamilifu suala la usalama wa taifa, akieleza kuwa amani, utulivu na heshima ya nchi hutegemea uimara wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Ameongeza kuwa nchi yoyote inapokosa chombo imara cha kusimamia usalama wake hupoteza heshima yake, huku akiipongeza wizara hiyo pamoja na jeshi kwa kuendelea kulinda amani na utulivu wa Tanzania.

samia-45 Rais Samia apongezwa kwa jitihada zake za kulinda amani na utulivu wa nchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *