Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi kikanda na kimataifa kwa kushiriki vikao mbalimbali vinavyolenga kuimarisha amani, ulinzi na usalama duniani.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 19, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo.
Dkt. Nyansaho amesema Wizara kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeendelea kushirikiana na nchi rafiki katika maeneo mbalimbali ikiwamo mafunzo ya kijeshi, mazoezi ya pamoja pamoja na utoaji wa misaada ya kitaalamu katika sekta ya ulinzi na usalama.
Amesema ushirikiano huo pia umehusisha taasisi za kimataifa na kikanda zikiwemo Umoja wa Mataifa(UN), Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) (SADC) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kupitia mafunzo, ubadilishanaji wa wataalamu na taarifa pamoja na utekelezaji wa operesheni mbalimbali za kiusalama.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania imeendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani katika kuimarisha sekta ya ulinzi na usalama, hatua ambayo amesema inalenga kuongeza uwezo wa kitaalamu, kuimarisha diplomasia ya ulinzi pamoja na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu.

