
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa onyo kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara wilayani humo, akiwataka kuzingatia mikataba na kukamilisha kazi kwa wakati.
Onyo hilo amelitoa wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya barabara aliyoifanya kwa kushirikiana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, ambapo alitembelea miradi inayotekelezwa na wakandarasi, wengi wao wakiwa kampuni za wazawa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mpogolo aliwakosoa baadhi ya wakandarasi kwa kuchelewesha miradi kwa visingizio visivyo na msingi, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi huku Serikali ikiwa tayari imeshatoa fedha kwaajili ya utekelezaji wa kazi hizo.
Aidha, alionya tabia ya baadhi ya wakandarasi kukaidi maelekezo ya wasimamizi wa miradi kutoka TARURA na TANROADS, wakitumia mwanya wa kufahamiana na baadhi ya viongozi wa juu.
Amesisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa, hasa vinapoambatana na ujenzi wa barabara chini ya viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Mpogolo pia ameeleza wasiwasi wake juu ya wakandarasi wanaochukua miradi mingi kwa wakati mmoja bila kuwa na uwezo wa kutosha wa rasilimali na vifaa, jambo linalosababisha baadhi yao kutelekeza miradi au kuchelewesha utekelezaji wake.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uchunguzi wa miradi kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wanaokiuka taratibu na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika Wilaya ya Ilala.
Katika ziara hiyo, Mpogolo ametaja baadhi ya barabara zilizokaguliwa kuwa ni pamoja na Halisi na Kimanga, zilizogharimu Sh. bilioni 1.7 zilizotolewa mwaka 2024.
Barabara nyingine ni Mafia, Masasi, Magila, Bondi na Muhonda, zilizogharimu Sh. bilioni 1.8 zilizotolewa mwaka 2025.
Pia amezitaja barabara za Mwanza, Livingstone, Nyamwezi, Kipati, Msikitini, Sharifushamba, Kigoma na Tunduru, zilizogharimu Sh.bilioni 1.9.
Mpogolo amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaoathiri ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha miundombinu na maisha ya wananchi.





