Kairuki: Wizara itaendeleza miradi 8 ya kimkakati

WhatsApp-Image-2026-04-30-at-02.18.23-1024x731 Kairuki: Wizara itaendeleza miradi 8 ya kimkakati

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, leo Alhamisi Aprili 30, 2025 amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, akieleza kuwa wizara itaendelea kutekeleza jumla ya miradi nane ya maendeleo yenye lengo la kuboresha sekta ya mawasiliano na teknolojia nchini.

Akiwasilisha mpango huo, Kairuki amesema miradi hiyo inajumuisha uendelezaji wa mkongo wa taifa wa mawasiliano, upanuzi wa huduma za mawasiliano vijijini, utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali pamoja na mradi wa anuani za makazi na posta kodi.

Aidha, wizara inapanga kujenga kituo kikuu na vituo vidogo vya kuendeleza ubunifu katika TEHAMA, kuongeza uwezo wa taasisi katika utekelezaji wa majukumu yake, kuhamasisha ubunifu pamoja na utengenezaji wa vifaa vya TEHAMA nchini.

Katika hatua nyingine, Kairuki amebainisha kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kuanzisha taasisi ya Taifa ya teknolojia ya kidijitali itakayojengwa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kukuza uchumi wa kidijitali.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kufikia matarajio makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote kwa ufanisi.

Mpango huo pia unaendana na malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/30, inayosisitiza maendeleo ya TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

WhatsApp-Image-2026-04-30-at-02.18.22-1024x731 Kairuki: Wizara itaendeleza miradi 8 ya kimkakati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *