Mavunde akabidhi mashamba kwa Wafanyabiashara wadogo Dodoma Mjini.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde jana amekabidhi mashamba ekari 4 mahsusi kwa kilimo cha mboga mboga na matunda kwa vikundi vya wafanyabiashara wadogo wa Twiga Group-Soko la Sabasaba na Mavunde Garden-Soko kuu Majengo Jijini Dodoma.

Mavunde amefanya makabidhiano hayo ya mashamba kwa vikundi hivyo katika mbuga ya Sogeambele,Kata ya Chihanga ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya uwezeshwaji wananchi kiuchumi.

“Nipo hapa leo kukabidhi mashamba haya kwa vikundi vya wafanyabiashara wadogo wa Soko kuu Majengo na Soko la Sabasaba.

Ni imani yangu kupitia mashamba haya mtaweza kuzalisha kwa wingi mazao ya mboga mboga na matunda na mkawa wasambazaji wakubwa wa mazao hayo ndani na nje ya mipaka ya Dodoma.

Mashamba haya yakitumika vizuri yanaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa vikundi vyenu na mimi nitakuwa nanyi bega kwa bega kuwapa msaada wowote unaohitajika ili muweze kufikia malengo yenu.

Pamoja na mashamba hayo lakini pia nitawasaidia mbegu bora kwa mazao ambayo mtachagua kuyapanda, gharama za maandalizi ya shamba na pia nimezungumza na watu wa TAHA ili baadaye tupate viosk mwendo kwa ajili ya kuuzia mazao yetu” Alisema Mavunde

Wakitoa shukrani zao viongozi wa vikundi hivyo Bi. Anna Nyigana (Twiga Soko Sabasaba) na Ndg. Yona Msanganzila (Mavunde Garden Majengo Sokoni) wamemshukuru Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa akiwawezesha kiuchumi na kuahidi kwamba watatumia mashamba hayo kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika vikundi vyao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *