Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeandika historia mpya kwa kutia saini Mkataba wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, utakaogharimu Dola za Marekani milioni 260 utakaotekelezwa kwa miaka miwili.

Fedha hizo ni mkopo wa Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Hispania na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi Euro milioni 30, ikiwa ni jitihada za Rais Suluhu Hassan katika kutekeleza adhma ya serikali ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo ilifanyika jana Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma kwa niaba ya serikali.

Kwa upande wa mzabuni ni Kampuni M/s China Civil Engineering Construction Cooperation kwa kushirikiana na China Railway Construction Cooperation Harbour Channel Engineering Bureau Group Co. Ltd. kwa gharama ya Sh. bilioni 195.66.

Akizungumza wakati wa halfa hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM– TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema mradi huo ni wa kuleta mabadiliko ya kweli.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Benki ya Dunia, Serikali ya Uholanzi na Serikali ya Hispania kwa kuguswa na changamoto za mafuriko katika Bonde la Msimbazi, kuwa na imani na maono yetu na kupelekea kuisaidia Serikali katika jitihada zake za kukabiliana na changamoto hii,” amesema.

Amesema mradi huo si tu kupanua mkondo wa mto bali pia kujenga msingi wa mustakabali bora wa kubadilisha eneo ambalo ni hatarishi kwa sasa na kuwa sehemu muhimu kwa uchumi na mazingira ya Dar es Salaam.

WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.40-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi

Amesema unalenga kunusuru maisha ya jamii kwa kuhamisha zaidi ya nyumba 3,000 kutoka maeneo hatarishi kwa mafuriko na kutoa fidia stahiki kwa usalama na ustawi wa wananchi.

Prof. Shemdoe amesema mradi huo, utatengeneza fursa kwa upatikanaji wa hekta 57 za ardhi salama iliyotengenezwa itatoa maeneo mapya kwaajili ya makazi na biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira.

Amesema pia ujenzi wa daraja jipya la jangwani lenye urefu wa mita 390 na karakana mpya ya mabasi ya mwendokasi eneo la Ubungo Maziwa kutaboresha kwa kiasi kikubwa usafiri na muingiliano ndani ya jiji.

Aidha, Prof. Shemdoe amesema kazi zitakazofanyika katika mradi huo ni ubomoaji wa nyumba zilizolipwa fidia na uhamishaji wa miundombinu ya huduma ili kupisha eneo la mradi.

Amesema pia uondoaji wa mimea, udongo wa juu na madampo yaliyopo, ukifuatiwa na upanuzi na kuongeza kina cha Mto Msimbazi.

Kadhalika watasafirisha udongo kutoka kwenye chanzo chake kwa ajili ya kutengeneza na kushindilia hekta 57 za ardhi kwa makazi na biashara salama.

Pia uimarishaji wa kingo za Mto Msimbazi na maeneo mapya ya ardhi yaliyotengenezwa, upandaji wa majani na mimea mingine kando ya kingo za mto na katika maeneo mapya ya makazi na biashara na ujenzi wa karakana mbili za utunzaji mchanga.

Aidha, amesema wanatambua uhamishaji wafanyabiashara waliopo katika eneo la mradi, ikiwamo wasafirishaji wa mizigo, soko la Kigogo na gereji, unahitaji mipango iliyoratibiwa na iliyo makini.

“Tunaiomba Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kusaidia kutafuta na kuandaa maeneo mbadala kwa ajili ya wafanyabiashara hawa ili kuhakikisha maisha yao ya kila siku hayaathiriki,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, amesema mradi utajenga daraja jipya eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na karakana mpya ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa.

Vilevile mradi unatarajiwa kuboresha maeneo korofi katika eneo la juu la Bonde pamoja na kuratibu shughuli za kibinadamu ili kudhibiti mmomonyoko wa udongo unaotuama eneo la chini na kusababisha mafuriko.

“Mradi ulianza rasmi mwezi Februari 2023 na utatekeleza kwa muda wa miaka sita,” amesisitiza na kuongeza kuwa; “Mpaka sasa mradi umeshalipa kiasi cha Sh. bilioni 73.69 kama fidia kwa waathirika wa mradi wapatao 2551 kwaajili ya kupisha uendelezaji wa eneo la chini la Bonde kundi hili ni la waathirika wanaoathirika na mafuriko.”

Amesema kundi la pili ni la waathirika wapatao 314 watakaoathirika na ujenzi wa matuta kwaajili ya maeneo salama ya makazi na biashara.

Viwango vya fidia kwa kundi la pili vimepelekwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupata idhini ya kufanya uthamini.

Ujenzi wa Daraja la Jangwani ulianza rasmi mwezi Mei 2025 chini ya usimamizi wa TANROADS.

Amesema Mkandarasi anayejenga daraja ni M/s China Communication Construc tion Company Ltd. kwa gharama ya Sh. bilioni 97.1, na Mtaalamu Mshauri wa Usimamizi ni Leporogo Specialist Engineers in JV with Afrisa Consulting Ltd and Dong Myeong Engineering Consultants & Architecture kwa gharama ya zaidi ya Sh.  bilioni 4.57 mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 34.

Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia (DW), Emma Philips, aliipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo mkubwa unaolenga kuboresha mazingira na kuokoa maisha ya wakazi wa jiji hilo.

WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.42-3-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.42-2-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.42-1-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.41-4-1-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.41-2-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.41-1-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.40-3-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.40-2-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi
WhatsApp-Image-2026-04-20-at-09.44.40-1-1024x683 Serikali yazindua mradi wa mageuzi makubwa mto Msimbazi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *