
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation wameungana kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutambua mchango wa mwanamke mjasiriamali mdogo wa mboga na matunda.
Kila mwaka tarehe 8 Machi, dunia huadhimisha Siku ya Wanawake ili kukumbusha juhudi zinazofanywa kumuinua mwanamke katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Katika maadhimisho ya mwaka huu, TAMWA na CRDB wameamua kutoa kipaumbele kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo za mbogamboga, wakitambua mchango wao katika kujikwamua kiuchumi.
Kupitia mpango wa IMBEJU, taasisi hizi zinawahamasisha wanawake kujiunga na vikundi na taasisi zinazowawezesha kupata elimu ya ujasiriamali pamoja na mitaji ya kukuza biashara zao. Wameeleza kuwa wanawake wengi wanafanya kazi kwa bidii lakini wanakosa maarifa sahihi ya biashara, hali inayosababisha kipato chao kubaki kidogo.
Aidha, maadhimisho ya mwaka huu yanakumbusha umuhimu wa Azimio la Beijing la mwaka 1995, ambalo lililenga kukuza usawa wa kijinsia kwa kuweka ajenda mbalimbali kama kupambana na umaskini, ukatili wa kijinsia, na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi na uongozi.
Licha ya juhudi hizo, bado changamoto zipo. Takwimu za mwaka 2025 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonyesha kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia yameongezeka, ambapo wanawake waliokumbwa na ukatili waliongezeka kutoka 21,466 mwaka 2022 hadi 25,420 mwaka 2023. Vilevile, watoto waliokumbwa na ukatili waliongezeka kutoka 12,163 hadi 15,301 katika kipindi hicho.
Kupitia tafiti na makala mbalimbali, TAMWA imebaini kuwa wanawake wengi wanaouza mboga hukumbana na changamoto nyingi, ikiwemo ukatili wa kijinsia, vikwazo masokoni na hata vitendo vya rushwa ya ngono. Wengine hulazimika kuamka alfajiri sana ili kutafuta bidhaa za kuuza.
Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ni njia muhimu ya kupunguza ukatili wa kijinsia. Ameongeza kuwa mwanamke akiwa na kipato cha uhakika hupunguza utegemezi na kuwa na uwezo wa kujilinda na kufanya maamuzi sahihi.
Kwa upande wao, TAMWA wametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali, kuimarisha mifumo ya kisheria, na kuhakikisha mazingira salama kwa wanawake na watoto.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Tunapotoa, tunapata,” inasisitiza umuhimu wa kushirikiana, kusaidiana na kutoa rasilimali kama maarifa, muda na msaada wa kifedha ili kuleta maendeleo chanya kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Naye Meneja wa Kusimamia na Kuwajengea Uwezo wa CRDB, Joshua Mwakalobo, amesema CRDB kwa kutambua kundi la wanawake na vijana wajasiriamali wasioweza kufikia huduma za benki wakaanzisha huduma ya IMBEJU.
Amesema lengo ni kufikia kundi hilo ambalo linaanzisha biashara lakini halina mtaji wa kutosha na wakati mwingine biashara zinakufa kwa kukosa mitaji.
“Kupitia CRDB Foundation ipo tayari kuwashika mkono wanawake na vijana wasiyo na vigezo vya kupata mikopo kikubwa tunahitaji wawe na utayari na uwajibikaji ili kumsaidia kufikia ndoto au malengo yake,” amesema Mwakalobo.


