
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wake mkubwa katika mashine za kisasa za upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwamo mashine za kisasa na mpya za MRI zilizonunuliwa Simens, nchini Ujerumani.
Shukrani hizo zimetolewa na Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka Hospitali hiyo Dkt. Joek Bwemelo, akisema MOI ina MRI aina ya Simens 1.5 Tesla ambayo tofauti na mashine nyingine, hii inahudumia wagonjwa 25- 35 kwa siku na ikigharimu zaidi ya Sh. bilioni 2. 6 za Kitanzania, akisema mashine hiyo ni kama mashine nyingine zote zinazotumika duniani katika masuala ya ubora na teknolojia ya karibuni zaidi.
“Muda wa kipimo hiki cha MRI unategemea sana aina ya uchunguzi, sehemu ya mwili inayopimwa na itifaki (sequence) zinazohitajika ili kupata picha zenye ubora wa juu kwaajili ya majibu sahihi na Mgonjwa anapimwa kadri ya vile ambavyo daktari atakuwa anasema, mfano kipimo cha kina cha Uti wa mgongo (Spine MRI) huchukua kati ya dakika 30 mpaka 60 kwenye mashine yoyote ile duniani,” amesema Dkt. Bwemelo.
Aidha, kutokana na mashine hizo kutengenezwa kwa mfumo wa duara, Dkt. Bwemelo amesema mashine hizo zimekuwa zikiwatia wengi wasiwasi, suala ambalo limezifanya MRI hizo kuja na kisikiliza muziki (Headphone) ambalo pia ni takwa la kisheria kwa kiwango cha usalama wa Kimataifa ili kuwalinda pia na sauti kubwa inayosikika kutoka kwenye uasili wa utendaji wa mashine zote za MRI.
Taasisi ya MOI imelazimika kueleza hayo kutokana na dhana potofu ambazo zimekuwa zikielezwa katika mitandao ya kijamii pamoja na maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa mfululizo, wengi wakihusisha mashine za MRI za Taasisi hiyo na uchakavu sambamba na kulalamika kuhusu muda mrefu unaotumika katika kupima wagonjwa sambamba na athari potofu zilizokuwa zikielezwa kuhusu uvaaji wa headphone
