
Na Mwandishi Wetu, Mara
MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameishukuru Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kuanzisha kambi ya matibabu mkoani humo, akisema uwepo wao umeleta faraja kubwa kwa wananchi, hususan katika matibabu ya majeraha yatokanayo na ajali.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 4, 2026 katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wakati wa ufunguzi rasmi wa kambi ya madaktari bingwa na bobezi wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu inayofanyika hospitalini hapo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtambi aliishukuru Wizara ya Afya kwa jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, na kuipongeza MOI kwa kuitikia wito huo.
Amesema hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu hayo.
“Tunaishukuru Wizara ya Afya kwa utaratibu wa kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na Taasisi ya MOI kuitikia wito huo… Uwepo wenu katika Mkoa huu si kuleta matibabu tu, bali mmeleta faraja kwa wananchi kwa kuwa mmewapunguzia usumbufu wa kwenda umbali mrefu kufuata matibabu,” amesema Mtambi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amepongeza uwepo wa MOI wilayani humo, akisema unasaidia kwa kiwango kikubwa kupambana na changamoto za matibabu ya majeraha yatokanayo na ajali za barabarani na magonjwa ya mifupa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, ameahidi kuwa taasisi hiyo itaweka kituo cha kudumu katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, ukanda wa Ziwa na hata mataifa jirani yanayokabiliwa na changamoto za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Dkt. Mpoki amesema katika siku mbili za uwepo wa madaktari bingwa wabobezi wa MOI katika hospitali hiyo kumewanufaisha zaidi ya wagonjwa 300 na wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji wa kibobezi.
Kambi ya matibabu ya kibingwa ya MOI katika hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inafanyika kuanzia Machi 2-6, 2026.




