
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TUME ya Ushindani (FCC) imesema itaendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria zake ili kuimarisha ulinzi wa walaji, kudhibiti bidhaa bandia na kuhakikisha ushindani wa haki unaochochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.
Hayo ameyasema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa wakati akifungua Semina ya kujengea uwezo waandishi wa habari jana Februari 24, 2026, jijini Dar es Salaam.
Khadija amesema marekebisho ya Sheria hayo yanalenga kumlinda mteja dhidi ya bidhaa zisizo na ubora, matangazo ya upotoshaji pamoja na vitendo vinavyokwenda kinyume na misingi ya ushindani wa haki.
Amesema moja ya vipaumbele vya tume hiyo ni kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti madhubuti wa bidhaa bandia zinazoingia sokoni, kwani huathiri afya za wananchi, hupunguza mapato ya Serikali na kuwakosesha wafanyabiashara halali fursa za kukuza biashara zao.

“Jukumu letu ni kuhakikisha uchumi unakua kwa misingi ya ushindani wa haki. Matokeo yake ni kuongezeka kwa uwekezaji na ajira kwa wananchi,” amesema Ngasongwa.
Aidha, amebainisha kuwa FCC itakuwa ikikutana mara kwa mara na waandishi wa habari na wadau mbalimbali ili kuwapatia taarifa sahihi kuhusu majukumu ya FCC pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Katika hatua nyingine, alisema kuna maboresho yanayofanyika kupitia TANOGA — Muunganiko wa Taasisi za Serikali za Udhibiti pamoja na Mawakala wa forodha kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa bidhaa zinazoingia nchini.

Khadija ameongeza kuwa taasisi hizo zitaingia katika mfumo wa kidijitali ili kupunguza mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watumishi na wateja, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kudhibiti mianya ya vitendo visivyo vya kiadilifu.
FCC itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi kuhakikisha mazingira ya biashara yanabaki kuwa salama, yenye ushindani wa haki na yenye manufaa kwa wananchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (Dar PC) Mary Geofrey, mbali na kuipongeza FCC kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha umma, aliiomba FCC kuendelea kutoa ushirikiano wa wanahabari wanapotala ufafanuzi wa mambo wanayokutana nayo kwenye jamii.


