MOI kuwa kinara matumizi ya teknolojia upasuaji wa saratani za ubongo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inakwenda kuandika historia mpya kwa kuwa ya kwanza katika nchi kusini mwa mwa Afrika kufanya kwa kuanza upasuaji wa saratani ya uvimbe wa Ubongo na Uti wa Mgongo kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayojuklikana kama ‘Fluoresence’.

Hayo yamebainishwa mapema wiki hii na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la tano la Kimataifa (MOI Neuro oncology Conference) la matibabu ya Saratani za ubongo na uti wa mgongo.

“Teknolojia hii inatumia aina fulani ya rangi (Fluorescein stain) ambayo inamwezesha daktari kwa kutumia darubini maalum, kuona eneo lenye uvimbe na kuweza kuutoa wote kwa ufanisi mkubwa…ni teknolojia mpya duaniani na sisi MOI tunakwenda kuwa taasisi ya kwanza Afrika Mashariki (EAC) na Kusini wa Afrika (SADC) kuanza kutibu wagonjwa kwa teknolojia hii,” alisema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa;

“Kongamano hili limeandaliwa na MOI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya cha Colorado cha nchini Marekani, limewaleta pamoja madaktari bingwa wa fani mbalimbali na wauguzi wabobezi kutoka maneo mbalimbali ya duniani.”

Aidha, Dkt. Mpoki alikishukuru Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha taasisi ya MOI inaendelea kuwa kituo cha umahiri cha matibabu ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu na kwamba anatambua mchango wao katika ujuzi na vifaa tiba.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa Kongamano hilo kutoka Chuo Kikuu cha Colorado Prof. Ryan Ormond, amesema teknolojia hiyo mpya inakwenda kuboresha hali ya matibabu ya saratani za ubongo, uti wa mgongo.

Pia aliongeza kuwa katika mkutano huo watabadilishana ujuzi katika matibabu ya mafuvu ya watoto chini ya miaka mitatu ambayo yana maumbo ambayo sio ya kawaida kama vile “kisogo bapa, uso kuwa upande (Plagiocephally) na fuvu kuchongoka kwenda juu (Scaphocephally) na matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa (Hydrocephally) kwa kupata matibabu sahihi ya kisasa yatakayowezesha kupona haraka.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo MOI Dkt. Lemeri Mchome, alisema kongamano hilo limewakutanisha wataalam kutoa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Africa na kwamba teknolojia hiyo mpya inakwenda kuleta mageuzi katika matibabu ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu nchini.

“Washiriki watajifunza mbinu za kisasa za matibabu ya saratani za ubongo, uti wa mgongo, na mshipa ya fahamu, lakini pia wataangazia matibabu ya kiharusi, na watoto wenye vichwa vikubwa sambamba na namna ya kuhudumia wagonjwa mahututi wa changamoto hizo,” alisema Dkt. Lemeri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *