Urambo na Kaliua zipo tayari kwa uwekezaji, umeme unaozalishwa unatosha- Ndejembi

Na Mwandishi Wetu, Tabora

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora zipo tayari kwa uwekezaji, hususan wa viwanda kwani umeme unaozalishwa katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Urambo unatosheleza na hata kuzidi mahitaji ya sasa.

Amesema hayo Jumamosi Februari 14, 2026, wakati akikagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Urambo na Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Uhuru – Urambo cha Megawati 24.

“Urambo ipo tayari kwa uwekezaji. Uwezo wa kituo cha Urambo ni megawati 24, lakini matumizi ya wilaya mbili za Kaliua na Urambo ni megawati 2.5 wakati wa mchana na wakati wa usiku ambacho ni kipindi watu wengi wanakuwa majumbani, kiwango cha juu cha matumizi ni megawati 7,” alisisitiza Ndejembi.

Ndejembi alisema lengo na dhamira ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kunakuwa na nishati ya umeme ya uhakika ili kuendelea kuchochea uwekezaji katika maeneo yote nchini, kwani nishati ya umeme ni kichocheo cha sekta zote.

WhatsApp-Image-2026-02-14-at-05.48.17-1024x682 Urambo na Kaliua zipo tayari kwa uwekezaji, umeme unaozalishwa unatosha- Ndejembi

Alisema wilaya za Urambo na Kaliua zimejikita zaidi katika kilimo hususan zao la Tumbaku, zao ambalo linahitaji kuongezewa thamani kupitia viwanda vilivyokuwa vinahitaji umeme wa uhakika.

Aidha, Ndejembi alisisitiza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa zaidi ya trilioni 1.9 kwa Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa ajili ya Mradi wa Gridi Imara kujenga vituo vya kupoza na njia za kusafirisha umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika, Ndejembi alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta ambaye alitoa eneo la hekari 20 lililotumika kujenga Kituo hicho cha Kupooza Umeme.

WhatsApp-Image-2026-02-14-at-05.48.23-1024x682 Urambo na Kaliua zipo tayari kwa uwekezaji, umeme unaozalishwa unatosha- Ndejembi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Urambo ulianza kutekelezwa Septemba 2021 kwa gharama ya Sh. bilioni 44. Kati ya hizo, Sh. bilioni 24 zilitumika kujenga njia ya kusafirisha umeme, bilioni 16 zimejenga kituo cha kupoza na Sh. bilioni 4 ilitumika kufidia wananchi waliopitwa na mradi.

Twange alisema kituo hicho kilianza kufanya kazi mwezi Machi 2025, ambapo ujenzi wa njia ya umeme pamoja na kituo cha kupokea na kupooza umeme vyote vimekamalika kwa asilimia 100.

WhatsApp-Image-2026-02-15-at-05.02.25-1-1024x682 Urambo na Kaliua zipo tayari kwa uwekezaji, umeme unaozalishwa unatosha- Ndejembi
WhatsApp-Image-2026-02-14-at-05.48.20-1024x682 Urambo na Kaliua zipo tayari kwa uwekezaji, umeme unaozalishwa unatosha- Ndejembi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *