Itaimarisha diplomasia, kukuza uchumi
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia, Tanja Fajon akiwa na ujumbe wake, amewasili nchini Aprili 13, 2023 kwa ziara ya siku tatu.
Ziara hiyo ya kikazi inalenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na Slovenia.
Lengo lingine la ziara hiyo ni kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake, Fajon alikutana, kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax, jijini Dodoma.
Mazungumzo yao yalijikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Slovenia.
Pia mazungumzo hayo yalihusisha uandaaji mazingira na utaratibu wa kusainiwa hati za makubaliano kwenye maeno mapya ya ushirikiano yaliyoainishwa.
Maeno mapya ya ushirikiano yaliyoibuliwa wakati wa mazungumzo hayo ni uzalishaji dawa (pharmaceuticals), usimamizi wa rasilimali maji na utunzaji wa mazingira.
Pia ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, sayansi na teknolojia, kilimo, Elimu, biashara na uwekezaji.
Mbali na hayo, Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kumweleza Fajon kuhusu juhudi ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mafanikio yaliyopatikana nchini.
Mafaniko hao ni matokeo ya juhudi hizo yakiwemo maridhiano ya kisiasa, kuimarika kwa demokrasia, haki za Banadamu, uhuru wa vyombo vya habari, uzingatiwaji usawa wa kijinsia katika maendeleo.
Kwa upande wake, Fajon aliipongeza serikali kwa hatua kubwa ya kuboresha mazingira ya demokrasia na utawala bora nchini, kuendelea kusimamia vyema maendeleo ya uchumi licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali duniani zinazodhoofisha ustawi wa uchumi.
Ziara hiyo ni muendelezo wa matokeo ya juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha ushirikiano wa Tanzania, mataifa mengine duniani.
Akiwa nchini, Fajon alikutana, kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa serikali.