Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amezindua magari mapya 25 kwaajili ya kusambazwa kwenye Ofisi za Maofisa Madini wakazi wa mikoa sambamba na kukabidhi magari hayo kwa maofisa hao.
Makabidhiano hayo ni mkakati wa kuimarisha usimamizi katika Sekta ya Madini hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri Mavunde uliofanyika jana Oktoba 22, 2024, amesema wizara imepanga kununua magari 89 na pikipiki 140 kama sehemu ya uboreshaji wa usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa hasa kwenye usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato na utoroshaji wa maduhuli.
Amesema kuwa, magari yaliyozinduliwa 25 ni awamu ya kwanza ya magari 89 yanayotarajiwa kuletwa sambamba na pikipiki 140 zitakazosambazwa kwenye ofisi za Maofisa Madini wakazi wa mikoa zilizopo nchi nzima.
Aidha, Mavunde ameelekeza magari yote kufungwa GPS kwaajili ya kuangalia mwenendo wake ili kuhakikisha yanatumika katika matumizi yaliyokusudiwa.
“Magari yote yatafungwa GPS ambapo Makao Makuu tutakuwa na uwezo wa kuona mwenendo wa magari kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye shughuli za ukusanyaji wa maduhuli na ukaguzi wa migodi ya madini,” amesisitiza.Katika hatua nyingine, Mavunde amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini kwa kuiongezea bajeti Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 mwaka 2023/2024 hadi shilingi bilioni 231 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amempongeza Waziri Mavunde kwa jitihada zake za usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwataka watendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha wanaonesha matokeo chanya kwenye utendaji kazi.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo sambamba na kuishukuru Wizara ya Madini kwa magari husika amesema kuwa magari yatatumika kama chachu ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwenye ongezeko la makusanyo ya maduhuli.
Amefafanua kuwa magari yote 85 yatakayonunuliwa yatagharimu zaidi ya Sh. bilioni 18.