Watu mil. 31.3 wajiandikisha kupiga kura uchaguzi Serikali za Mitaa 

Na Salha Msangi, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema wapiga kura 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha watu 32,987,579 Mkoa wa Pwani ukiongoza.

Kati ya waliojiandikisha kwenye daftari wanaume ni 15,236,772 sawa na asilimia 48.71 na wanawake ni 16,045,559 sawa na asilimia 51.29.

Mchengerwa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa tathmini ya uandikishaji wa wapiga kura kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 uliofanyika kwa siku 10 kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024.

“Mwenendo wa uandikishaji kwa kila siku kwa kipindi cha siku 10 ulikadiriwa kuandikisha wastani wa asilimia 10 kwa siku ili kufikia lengo lililokusudiwa,”amesema.

Amesema siku ya kwanza waliandikishwa watu 3,882,994 sawa na asilimia 11.82 ya lengo la siku la kuandikisha kwa asilimia 10 na siku ya pili waliandikishwa watu 2,554,375 sawa na asilimia 7.78 ya lengo la siku.

Ameongeza kuwa siku ya tatu waliandikishwa watu 2,660,084 sawa na asilimia 8.10, siku ya nne waliandikishwa watu 2,544,844 sawa na asilimia 7.75.

“Siku ya tano waliandikishwa watu 2,460,664 sawa na asilimia 7.46, Siku ya sita waliandikishwa watu 2,472,605 sawa na asilimia 7.50, Siku ya saba waliandikishwa watu 2,971,219 sawa na asilimia 9.01.

“Siku ya nane waliandikishwa watu 3,409,211 sawa na asilimia 10.33, Siku ya tisa waliandikishwa watu 3,813,999 sawa na asilimia 11.56 na Siku ya kumi waliandikishwa watu 4,512,336 sawa na asilimia 13.68 ya lengo la siku,”amesema.

Mchengerwa amesema kwa ujumla mikoa yote 26 imefanya kazi nzuri katika zoezi hilo la uandikishaji ambapo matokeo yanaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 ambapo waliandikishwa wapiga kura 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *