Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Tanzania inakwenda kuwa kitovu cha Tiba Utalii, kutoa huduma za afya kwa wagonjwa maalumu wa ndani na nje ya nchi.
Mwalimu aliyasema hayo jana baada ya kufungua mradi wa kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wa kimataifa iliyopo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) itakayotoa huduma za kliniki kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.
“Haya tunayoyashuhudia leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Djt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya nchini.
“Niipongeze taasisi ya MOI chini ya Prof. Abel Makubi na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Charles Mkony kwa kazi nzuri ya kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema.
Aliwaomba Watanzania wenye uhitaji wa tiba kwa haraka wakiwemo watumishi au wafanyabiashara waende MOI ambapo ndani ya saa mawili unamaliza kila kitu na kuendelea na shughuli zako.
Aliitaka MOI iendeshe kliniki hiyo kwa ubia na wawekezaji wengine ili kuboresha huduma.
“Ni jambo zuri sana ambalo mmelianzisha lakini tusije kukwama njiani hivyo tushirikiane na wadau wengine ili huduma hii iendelee.
“Ni matarajio yangu kliniki hii ya wagonjwa maalumu na wagonjwa wa kimataifa itakuwa ya mfano ambayo itakua kivutio kikubwa kwa wagonjwa kutoka katika mataifa mbalimbali,” aliongeza.
Mwalimu alsema, kutokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, vifaa tiba na wataalamu, MOl imefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjuwa kwenda nje ya nchi.
Hivi sasa, asilimia 99 ya huduma za mifupa zinapatikana nchini na asilimia 97 ya huduma za kibingwa za ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zinapatikana nchini.
Alizitaka hospitali nyingine kuwa na huduma za haraka kwani Watanzania wanataka huduma bora kwa kuzingatia weledi, maadili na taaluma wakati wa kumuhudumia mgonjwa kwa kuanza na mapokezi mazuri.
Aliwataka Watanzania kuzingatia ulaji bora, kupunguza matumizi ya sukari nyingi, chumvi na mafuta mengi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
Magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la juu la damu (Presha) na kisukari kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka Tanzania.
Alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kusikiliza kilio cha Watanzania na kuboreha huduma za afya ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya majengo, vifaa, vifaa tiba na sasa tunakwenda kuwa kitovu cha Tiba Utalii.