Samia atoa Shs. bilioni 9 kusomesha wataalamu bingwa bobezi wa afya 601

Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kiasi cha Shs. bilioni 9 kwa ajili ya kusomesha wataalamu bingwa na bobezi 601 katika fani mbalimbali za afya ili kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Jumatano, Novemba 29, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Rais Samia wa kuongeza wataalamu bingwa na bobezi wa afya nchini kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha kiasi cha Shs. bilioni 9 kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za Sekta ya Afya ambapo fedha hizo ni muendelelezo wa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais,” alisema Waziri Ummy.

Ummy alisema, fedha hizo zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 601 sawa na 92% ya waombaji ambao walikidhi vigezo vya kusomea utaalamu wa ubingwa na bobezi wa fani mbalimbali za Sekta ya Afya.

“Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo na posho ya utafiti kwa watakaofadhiliwa ndani ya nchi na kwa wanaokwenda kusoma vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada, posho ya kujikimu wakiwa masomoni (Stipend), nauli ya kwenda na kurudi pamoja na posho ya utafiti.” alisema.

Waziri Ummy aliwataka wataalamu wote waliopata ufadhili huo wa mwaka 2023/2024 kukamilisha taratibu za kujaza mikataba ya ufadhili kama ishara ya kukubali ufadhili huo.

Alisema kuwa muda wa kujaza mikataba ya ufadhili ni kuanzia Novemba 29, 2023 hadi 12 Disemba, 2023 na nakala ya mikataba hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya na pia itatumwa kwa barua pepe kwenye anuani za barua walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *