Na Mwandishi Wetu, Njombe
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umetoa sh. bilioni moja kutekeleza miradi ya elimu Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe.
Fedha hizo zimetolewa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia tangu aingie madarakani.
Dkt. Dugange aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chalowe wilayani humo baada ya kuzindua vyumba vitatu vya madarasa, matundu matatu ya vyoo yenye thamani ya sh. milioni 82.
Madarasa na vyoo hivyo vimejingwa kupitia Mradi wa kuimarisha ufundishaji, ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania Bara.
“Kipekee sana tunamshukuru Rais Dkt. Samia, ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, Wilaya ya Wanging’ombe imenufaika na miradi ya elimu.
“Zaidi ya sh. bilioni moja zimekuja na kutekelezaji miradi ya elimu msingi na sekondari. Kwetu haya ni mafanikio makubwa sana, Kata ya Igwachanya ilikua na shule moja ya sekondari ikawa inazidiwa na idadi ya wanafunzi.
“Serikali ya Rais Dkt. Samia iliamua kuleta sh. milioni 583 kwa ajili ya sekondari nyingine ya Mtapa hivyo kata hii itakuwa na sekondari mbili, kumaliza changamoto ya mrundikano wa wanafunzi,” alisema.
Alieleza kuwa, Shule ya Msingi Chalowe ilikuwa na changamoto ya madarasa kwani yaliyokuwepo awali yalikuwa chakavu.
Kukamilika kwa vyumba vitatu kutaondoa changamoto iliyokuwepo na kusisitiza kuwa, serikali ya awamu ya sita imedhamiria kumaliza kero ya miundombinu ya elimu.