Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Halmashauri mbili kuanzia Novemba 20, 2023 ili kupisha uchunguzi.
Wakurugenzi hao ni ButamoNdalahwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani na Lena Nkaya wa Halmashauri wa Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Nteghenjwa Hosseah, alisema Mchengerwa alifikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma zao.
Alisema taarifa za awali zinasema, timu iliyoundwa kuchunguza tuhuma zao, imebaini Wakurugenzi hao walishindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika halmashauri zao kwa nyakati tofauti.
Timu hiyo iliundwa na Katibu Mkuu kwa maelekezo ya Mchengerwa na kubaini mapungufu hivyo Wakurugenzi hao wamesimamishwa kazi kwa kuzingatia Kanuni ya 37 (1) na 38 (1) ya Kanuni za Utumishi wa umma mwaka 2022 ili kupisha uchunguzi wa kina.
Hata hivyo, alisisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, kusimamia miradi ya maendeleo.
Mchengerwa alisema, hatasita kuchukua hatua stahiki kwa atakayethibitika kutenda kinyume.