Samia: Tutaendelea kuhubiri maridhiano

*Asisitiza amani, upendo, umoja wa kitaifa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuhubiri haki na maridhiano kama msingi wa amani katika nchi, kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii, maarifa ili kujiletea maendeleo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliyasema hayo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia na kusisitiza kuwa, bila kazi hakuna Taifa.

Dkt. Biteko alikuwa katika Sherehe za kumpongeza Mhashamu Askofu Mkuu (mstaafu) Paul Ruzoka, iliyofanyika Jimbo Kuu Kanisa Katoliki Tabora.

Alisema Serikali itaendelea kulinda kwa nguvu uhuru wa wananchi kutoa mawazo, imani na uchaguzi katika dini ili kuhakikisha kunakuwa na amani, utulivu, uhuru huo wa kuabudu na kutoa mawazo uwepo muda wote.

“Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan muda wote amekuwa akisisitiza haki kwa wananchi na ili kuishi katika misingi ya utangamano haki lazima itawale.

“Pia Rais Dkt. Samia anataka wananchi wasikilizwe; tunaweza kutofautiana katika maoni, mitazamo lakini kamwe tusivunje umoja wa kitaifa.

“Tuwaunganishe Watanzania, tupambane kuwaondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea nafuu kubwa ya maisha,” alisema Dkt. Biteko

Aliongeza kuwa, msisitizo wa Rais Dkt. Samia ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila kuangalia tofauti zao ikiwemo maji, barabara, umeme, shule, lengo  lake ni kuwaunganisha wananchi ili kuleta umoja nchini.

Alieleza kuwa, Rais Dkt. Samia yupo tayari muda wote kushirikiana na taasisi za dini nchini ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko alisema Rais Dkt. Samia aliahidi kuendelea, kutoa ushirikiano kwa Askofu Mkuu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa kama alivyofanya kwa mtangulizi wake Mhasham Askofu Mkuu mstaafu Ruzoka.

Kwa upande wake, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa na Mhashamu Askofu Mkuu mstaafu Ruzoka walishukuru kwa ushirikiano ambao Serikali imeendelea kuutoa kwao na kuahidi kuwapa ushirikiano zaidi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, chama akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian na Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala. Pia walikuwepo viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini kutoka ndani na nje ya nchi, waumini wa Kanisa hilo kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *