Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema bado kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa katika ofisi za umma.
Hali hiyo kusababisha wananchi wengi kushindwa kuzifikia huduma wanazozihitaji.
Simbachawene aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) unaofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma.
Alisema rushwa ndogondogo bado zipo na zinawakera wananchi hivyo lazima kuwe na mikakati ya kuhakikisha zinazuiliwa.
“Bado suala la rushwa ndogondogo ni tatizo sana kwa wananchi wetu, huko ndiko yapo malalamiko mengi ya watu kutokana na rushwa hiyo kuwanyima fursa ya kupata huduma.
“Huduma hizo ni pamoja na elimu ngazi za chini kati hadi vyuo vikuu, huduma za afya, kodi na leseni ambapo kuna utaratibu mgumu, ukilitimba katika utoaji huduma ili watu watoe rushwa ndipo wahudumiwe,” alisema.
Alieleza kuwa, ipo haja ya kutengeneza sheria za kuwashughulikia viongozi walioshiriki masuala ya rushwa wanapostaafu ili kutoa funzo kwa wengine.
“Mtu anapostaafu kama alishiriki katika uozo lazima ashughulikiwe, tukifanya hivyo tutakuwa tunatoa somo kwa viongozi wengine.
“Tusiposhughulikiana tutakuwa hatusemi ukweli kwa Taifa letu kwasababu rushwa bado ni tatizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Rashid Hamduni, alisema mwaka wa fedha uliopita taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa sh. bilioni 171.9
“Mafanikio tuliyoyapata mwaka wa fedha uliopita, TAKUKURU kwa kutumia vyombo vya uchunguzi imefanikiwa kuokoa zaidi ya sh.bilioni 171.
“Fedha hizo kama zisingefuatiliwa zingeishia mikononi mwa watu na kufanyiwa ubadhilifu,” alisema CP Hamduni
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha uongozi imara kwa vitendo.
“Tunampongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuonyesha uongozi imara kwa vitendo ambapo amekuwa akiongeza bajeti ya taasisi zinazosimamia haki na demokrasia ili zifanye kazi kwa weledi,” alisema.