- Balozi Bwana amrithi Meje Jenerali Milanzi Afrika Kusini
- Mkenyenge aenda NIC, Doriye kupangiwa majukumu mengine
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Sukuhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amevunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanzia Novemba 7, 2023.
Bodi ya TCRA ilikuwa inaongozwa na Mhandisi Othman Sharif Khatib kama mwenyekiti, wakati makamu wake alikuwa Khalfan S. Saleh.
Wajumbe wa Bodi hiyo walikuwa Dkt. Mzee Suleiman Mndewa, Dkt. Fatuma Simba Ikuja, Dkt. Abdallah Batenga Katunzi na Bi. Rehema Jessica Khalid.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus alieleza kuwa licha ya kuvunja bodi hiyo, Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi.
Alisema Rais Samia amemteua Balozi James Gilawa Bwana kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika kusini akichukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Gaudence Salim Milanzi ambaye amestaafu.
Alisema amemteua Balozi Said Hussein Massoro kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kuwait akichukua nafasi ya Balozi Said Shaib Mussa ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aidha, alisema amemteua Kaimu Abdi Mkeyenge kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambapo kabla ya uteuzi huo Mkeyenge alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Alisema, Mkeyenge anachukua nafasi ya Dkt. Elirehema Doriye ambaye atapangiwa kazi nyingine.