Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema imeendelea kuweka mikakati na mipango mahsusi ili kuhakikisha inarejesha uoto wa asili katika ardhi takribani hekta milioni 5.2 ifikapo 2030.
Hayo yamesemwa Novemba 6, 2023 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua warsha ya Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI), kutoka mataifa 10 duniani inayotekeleza Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai ulimwenguni.
Maganga alisema uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea maliasili ikiwemo misitu, bahari,maziwa, mito, ardhi oevu, wanyamapori na ardhi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini, hata hivyo matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hizo yameleta tishio la uwepo wa rasilimali hizo.
“Upotevu wa bioanuai ikiwa ni pamoja na viumbe wengine wa majini unachochewa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu ikiwemo kilimo na matumizi mengine ya ardhi yasiyo endelevu….Tumeanzisha programu mbalimbali za urejeshaji wa uoto wa asili ikiwemo kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya nchi” alisema Maganga.
Maganga alisema inakadiriwa duniani kote takribani ekari milioni 18.7 za misitu hupotea kila mwaka na kutokana na umuhimu wa urejeshaji wa ardhi, Tanzania imetenga ukubwa wa eneo takriban asilimia 40 ya eneo lote la ardhi ikijumuisha 6.5% ya bahari na 33% ya maeneo ya nchi kavu.
Alisema katika kuunga mkono juhudi za kidunia za urejeshaji wa ardhi na uhifadhi wa mazingira, Tanzania imezindua sera mpya ya Taifa ya Mazingira (2022) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) ambao umezingatia mipango shirikishi ya usimamizi wa mazingira katika ngazi zote.
Alisema lengo la mradi huo wa TRI ni kuimarisha usimamizi wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo-ikolojia na jamii kwa na ni sehemu ya mradi mkubwa wa kidunia unaotekelezwa katika nchi 11 duniani ikiwemo Tanzania
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa alisema warsha hiyo ya siku tano imekusudia kuwakutanisha wataalamu hao na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa miradi ya urejeshaji katika mataifa 10 duniani na kuanisha mbinu za upatikanaji wa rasilimali muhimu za usimamizi wa miradi hiyo.
“Warsha hii imeshirikisha wataalamu wanaotekeleza mradi wa TRI na kwa pamoja tutajengeana uwezo, mbinu na mikakati mbadala yenye uhalisia na nadharia ya kila nchi kutoka katika katika ukanda katika namna inavyotekeleza na kusimamia miradi ya TRI” alisema Kemilembe.
Kwa upande wake, Meneja Tathimini na Ufualitiaji wa Shirika la Kimataifa la Mazingira (IUCN) Tanzania, Dkt. Francis Musau aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi Wa urejeshaji na kuwa kuitaja kuwa ni miongoni mwa nchi ya mfano inayotekeleza vyema miradi hiyo ya TRI.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda alisema malengo ya mradi huo ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo-ikolojia na jamii nchini.
Alisema mradi huo hapa nchini unatekelezwa katika katika Mikoa 5 Halamshauri 7, Kata 18 na Vijiji 54 ambapo eneo la mradi linajumuisha mifumo ikolojia ya mabonde matatu ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa.
Alizitaja Halmashauri zinazotekeleza mradi huo ni pamoja na Halmashauri za Wilaya za Iringa Vijijini (Iringa), Mbeya na Mbarali (Mbeya), Wanging’ombe (Njombe), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa), Tanganyika, na Mpimbwe (Katavi).
Mradi unafadhiliwa wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF). Nchi nyingine zinazotekeleza mradi huo ni pamoja na Cameroon, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Guinnea Bissau, Kenya, Myanmar, Pakistan, Sao Tome& Principe.