Sera mpya Elimu yafuta darasa la 7

*Elimu ya lazima sasa miaka 10

*Ili usomee Ualimu uhitimu VI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI imefanya maboresho katika baadhi ya maeneo kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo.

Lengo ni kutoa elimu ya ujuzi badala ya elimu ya taaluma pekee ambapo elimu ya lazima itakuwa miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana bungeni jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023, Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Alisema utekelezaji wa maboresho hayo utaanza mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala yake kuanza kufanyika tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari.

Alieleza kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika changamoto mbalimbali zikiwemo mfumo wa elimu kujikita zaidi kwenye elimu ya jumla, kukosa fursa za elimu, mafunzo kwa kuzingatia mahitaji, njia mbalimbali za ujifunzaji kutokidhi kulingana na mazingira.

Alitaja changamoto nyingine ni mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu, upungufu wa nguvu kazi.

“Changamoto hizo zilizaa hitaji la kuboresha sera yetu ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa, wakati ujao,” alieleza.

Akifafanua maeneo yaliyoboreshwa katika sera hiyo ambayo tarehe ya uzinduzi wake itatangazwa baadaye, Majaliwa alisema Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikilinganishwa na sera iliyopita kwa kuongeza fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi, mafunzo ya ufundi stadi) ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.

Elimu ya Ualimu nayo itaanza kutolewa kwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita na kuendelea.

“Mafunzo ya ualimu yatajumuisha mwaka mmoja wa mafunzo chini ya uangalizi (internship) baada ya kuhitimu mafunzo tarajali,” aliongeza.

Alifafanua kuwa, maeneo yaliyoboreshwa ni mfumo wa upimaji na tathmini ambao utazingatia mahiri zinazohitajika kila ngazi ili kuwa na upimaji endelevu na matumizi ya mbinu mbalimbali za upimaji, tathmini ya maendeleo ya wanafunzi katika kujifunza.

“Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya msingi na Sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana.

“Pia Serikali itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji, vipawa mbalimbali,” alisema.

Wakati huohuo, Majaliwa alisema Wizara yenye dhamana na elimu ina wajibu wa kuandaa mikakati na mipango ya sekta, kutafuta rasilimali mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji,  kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera hiyo.

Pia Wizara yenye dhamana na TAMISEMI itakuwa na wajibu wa kuratibu na kusimamia Tawala za Mikoa zenye jukumu la kutekeleza sera kwa kutoa elimu na mafunzo katika ngazi ya awali, msingi, sekondari na Wizara yenye dhamana na Utumishi itahusika na upatikanaji wa rasilimali watu.

Majaliwa aliongeza kuwa, Wizara yenye dhamana na fedha itahusika na utafutaji, upatikanaji rasilimali fedha, Tawala za Mikoa zitasimamia utekelezaji wa sera na miongozo ya utoaji elimu, mafunzo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaendelea na utekelezaji wa sera hivyo kutoa huduma za elimu ili kuwafikia walengwa wote.

“Katika kutimiza azma hiyo, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo mashirika ya kidini, yasiyo ya Serikali na wadau wengine katika kuboresha upatikanaji, utoaji elimu na mafunzo,” alieleza.

Alisema mgawanyo wa majukumu utafuata mifumo ya kitaasisi iliyojengwa kisheria kadri ya utaratibu wa Serikali ambapo Wizara yenye dhamana ya elimu, taasisi zake itaendelea na wajibu wa kusimamia, kuratibu na kuimarisha upatikanaji, utoaji elimu, mafunzo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *