*Ndoto ya Rais Samia inaenda kutimia
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MUSWADA wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa unatarajiwa kuwasilishwa bungeni jijini Dodoma leo.
Awali muswada huo ulikwama Februari, 2023 kwa hoja iliyotolewa na Bunge juu ya kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha za kutekeleza mpango huo.
Muswada huo ni ndoto ya serikali ya miaka mingi ambapo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha huduma bora za afya.
Huduma hizo zimeboreshwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi msingi kwa kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za afya karibu zaidi na maeneo yao.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Wizara ya Afya, Englibert Kayombo, alisema Serikali kupitia Wizara yhiyo, wadau wa sekta na wataalam wengine tayari wamefanyia kazi hoja zilizoibuliwa na Bunge.
Senina zimefanyika kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote .
“Tulipokea maoni yao, kuyafanyia kazi, kesho (leo), wananchi watege macho na masikio yao bungeni kujua nini ambacho Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu atawasilisha bungeni,” alisema.
Alieleza kuwa, kupitishwa kwa Muswada huu kutawezesha kila Mtanzania kuwa ndani ya mfumo wa Bima ya Afya hatua itakayoboresha zaidi upatikanaji wa huduma za matibabu bila kuwa na kiwazo cha fedha.
“Serikali yetu ni sikivu sana, imefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi.
“Yaliyomo ndani ya muswada huo yamelenga kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo cha fedha,” alisema Kayombo.
Kuhusu gharama za vifurushi, Kayombo alisema baada ya Muswada huo kupita na kuwa sheria, kanuni zitatungwa ili kuratibu suala ya gharama za vifurushi.
Alisea uchambuzi utafanyika ili vifurushi viwe vya gharama nafuu na kila mwananchi aweze kuwa na bima ya afya.
Aliongeza kuwa, upande wa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya kutoa huduma kwa wananchi kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote.
Serikali imeboresha ubora wa huduma katika vituo vyake vya kutolea huduma, upatikanaji wa dawa, ununuzi na usimikaji wa vifaa, vifaa tiba, ajira za watumishi.
“Kwa sasa nchi iko mbali sana katika utoaji huduma, tuna vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa, huduma nyingi za kibingwa zinapatikana nchini.
“Pia huduma za afya zimesogezwa sana kwa wananchi hivyo kama nchi tupo tayari kutekeleza hili, nia na uwezo wa kufanya hivyo tunao” aliongeza Kayombo.