*Itaimarisha biashara, uwekezaji
*Kuja na wawekezaji kampuni 12
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia leo hadi Novemba Mosi, 2023.
Ziara hiyo imelenga kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya matafa hayo, pia kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilisema katika ziara hiyo, Rais Steinmeier ataongozana na viongozi wengine wa Serikali, wawekezaji wa makampuni makubwa 12.
Ujumbe huo utawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
Akiwa nchini, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu, jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2023.
Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea mambo muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.
Pia viongozi hao watapata fursa ya kushiriki Jukwaa la Biashara, litashirikisha wafanyabiashara, wawekezaji kutoka nchi hizo ambalo lmeandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Hoteli ya Hyatt Regency.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao watapokea taarifa iliyojadiliwa na jukwaa hilo. Siku hiyo hiyo, Rais Steinmeier anatarajiwa kuonana, kuzungumza na vijana wajasiriamali wa Kitanzania.
Vijana hao ni wale wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia mpya hususan matumizi ya akili bandia ambao wanafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.
Pia Rais Steinmeier atatembelea Kiwanda cha Twiga Cement jijini Dar es Salaam kinachoendeshwa kwa ubia na Kampuni ya Scancem International ya Ujerumani.
Novemba Mosi, 2023, Rais Stenmeier atasafiri kwenda Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma ambako atatembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji na Shule ya Msingi ya Majimaji.
Hii ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
Tanzania na Ujerumani zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu muda mrefu ambapo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati hususan biashara na uwekezaji.
Sekta nyingine ni maji, afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, uhifadhi wa bioanuai, usimamizi wa fedha, utalii pamoja na malikale na utamaduni.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka.
Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni kahawa, tumbaku, pamba, asali, samaki, nta na vito vya thamani. Pia Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani wastani wa Dola za Marekani milioni 237.43 kwa mwaka.
Pia bidhaa kuu zinazoagizwa kutoka Ujerumani ni dawa, vifaa tiba, mafuta (manukato, vipodozi) magari, vifaa na mashine za umeme.
Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini ambapo kwa mujibu wa TIC, hadi kufikia Agosti, 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 ilisajiliwa, kutoa fursa za ajira 16,121.
Upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300.00 ambayo imezalisha ajira 905.
Kampuni za Kijerumani zilizowekeza nchini zinajihusisha zaidi na sekta za kilimo, viwanda, nishati mbadala, ujenzi, utalii sanaa na utamaduni.
Kufanyika kwa ziara hiyo ni ushahidi tosha kuwa Diplomasia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia inazidi kupaa.