Waziri Jafo, KEPO wajadili teknolojia usimamizi wa taka

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo, amekutana, kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Shirika la Mazingira la Korea (KEPO) Dkt. Yoon, Young-bong, jijini Incheon, Korea Kusini.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Jafo ameeleza nia ya Tanzania kuanzisha ushirikiano katika sekta ya utunzaji wa mazingira hasa teknolojia ya usimamizi wa taka.

Kupitia kikao hicho akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini,  Togolani Mavura, viongozi hao walijadili kubadilishana uzoefu wa kisera upande wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika hilo Dkt. Young-bong, alimueleza Dkt. Jafo kuwa wako tayari kushirikiana na Tanzania katika usimamizi wa taka.

Viongozi hao walikubaliana kuendeleza mazungumzo katika kuelekea hatua za utekelezaji wa ushirikiano huo unaotarajiwa kusaidia utunzaji wa mazingira nchini.

Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo imeendelea kuibua miradi ya kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia taka nchini.

Alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira (2022-2032) ambao pamoja na mambo mengine changamoto za hifadhi ya mazingira, hatua za kukabiliana nazo zimeainishwa.

Pia ofisi hiyo kwa kushirikiana na wadau imeandaa Mwongozo wa Usimamizi Endelevu wa Taka kwa kuzingatia dhana ya ‘Punguza Uzalishaji wa Taka, Tumia tena na Rejereza’

Katika ziara hiyo ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano katika masuala ya mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Jafo ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais, Dustan Shimbo.

Itakumbukwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha diplomasia na mataifa mbalimbali duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *