Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Tanzania inashina nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga kwa kupata alama 86.7.
Tanzania inatanguliwa na Nigeria, Kenya na Ivory Coast katika ukaguzi uliofanyika Mei, 2023.
Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 20 ya TCAA kwenye ukumbi wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Katika ukaguzi mwingine wa uwezo wa nchi kiusalama uliofanywa na Shirika la ICAO, viwanja vya ndege vya KIA, Zanzibar na JNIA Dar es Salaam vilikaguliwa na kupata alama 86.7.
“Hatua hiyo imewezesha nchi yetu kushika nafasi ya nne Barani Afrika ikitanguliwa na nchi za Nigeria, Kenya na Ivory Coast.
“Huu ni ushahidi tosha kwamba uwezo wa nchi yetu katika kudhibiti usalama wa anga unaimarika,” alisema.
Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi huo, alisema Tanzania imeweza kuongeza uwezo wa udhibiti wa sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini kwa viwango vya kimataifa.
“Kupitia kaguzi za Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini, imeongeza uwezo kutoka asilimia 37.8 mwaka 2013 hadi asilimia 69.04 mwaka 2019.
“Kutokana na ufaulu huo, ICAO imetoa ufadhili wa dola za Marekani milioni moja zilizotumika kwenye mradi wa kuboresha uwezo wa usimamizi wa anga letu,” alieleza.
Mafanikio mengine ni ongezeko la mchango wa sekta ya uchukuzi katika Pato la Taifa akisema katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo, sekta hiyo ilichangia asilimia 8.2 ya pato la Taifa mwaka 2022.
Sekta hiyo imeendelea kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo sekta za utalii, biashara na nyinginezo.
Aliongeza kuwa, jitihada mbalimbali za Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga zimesaidia kuongeza idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa nchini.
Akitolea mfano wa ongezeko hilo katika kipindi cha miaka 10, alisema idadi ya abiria imeongezeka kutoka 1,662,452 mwaka 2003 hadi 4,614,380 mwaka 2023, mizigo imeongezeka kutoka tani 33,255 mwaka 2003 hadi tani 55,806.20 mwaka 2023.
AwaliWaziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema anaamini ukifanyika ukaguzi mwingine, Tanzania itafikisha alama zaidi ya 90.
Alisema Serikali inaendelea na ufungaji mitambo ya kuongoza ndege kwenye viwanja vya ndege vilivyoko Pemba, KIA, Mwanza, Songwe na Arusha.
“Ninaamini sekta hii itapiga hatua kwa kasi zaidi katika kipindi kifupi kijacho,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema taasisi hiyo ilianzishwa Novemba Mosi, 2003, inatoa huduma za uongozaji ndege katika viwanja 15 nchini.
Viwanja hivyo ni Arusha, Geita, Dodoma, Kigoma, Mtwara, Mwanza, Zanzibar, Pemba, Dar es Salaam, Songea, Songwe, Iringa, Tanga, Tabora na Bukoba ambako hivi karibuni wamefunga mitambo ya kuongoza marubani wakati wa hali mbaya ya hewa.