Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda hasa vya dawa, vifaa tiba.
Rais Dkt. Samia ameendelea kutoa fedha za uwekezaji katika sekta ya viwanda na miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa awamu ya tano inatekelezwa.
Mwalimu aliyasema hayo mkoani Njombe wakati akikagua uzalishaji katika kiwanda cha mipira ya mikono (gloves) kilichopo Idofi, mkoani humo.
Kiwanda hicho kinasimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ambacho leo kinatarajia kuwekwa jiwe la misingi na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.
Alisema ujenzi na uzalishaji katika kiwanda hicho unaridhisha na kukidhi mahitaji.
Aliongeza kuwa, uwekezaji wa viwanda vya dawa, vifaa tiba unaofanywa na serikali unaenda kupunguza uagizaji bidhaa nje ya nchi na matumizi ya fedha za kigeni.
Katika hatua ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Rais Dkt. Samia alikuta kikiwa asilimia 30, sasa kipo asilimia 90.
“Lengo la serikali ya Rais Dkt. Samia ni kufikia asilimia 50 kutoka asilimia 15 iliyopo sasa katika ununuzi wa bidhaa za afya ndani ya nchi kufikia 2030,” alisema.
Alisema kwa sasa vifaa vya afya kwa asilimia 85 vinanunuliwa nje ya nchi, zipo changamoto ikiwemo ya kusubiri bidhaa miezi tisa hadi kufika nchini, kusababisha uhaba wa dawa, ongezeko la matumizi ya fedha za kigeni.
Mwalimu alisisitiza kuwa, kwa sasa kuna viwanda 30 vya dawa, vifaa tiba vya ndani na kati ya hivyo 11 vinafanya kazi ambapo tayari serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni 11 ya uendelezaji kiwanda hicho na kudhamiri kuongeza uzalishaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.
“Niipongeze sana Bodi ya MSD, tunazungumzia bidhaa za afya za watu, lazima kujiridhidhisha wamefanya hivyo na kiwanda kiko vizuri ambapo tutakifungua kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisisitiza.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alisema kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa awali na kinatararajiwa kukamilika mwishoni mwa 2023.
Alisema kiwanda hicho hadi kukamilika kwake kitagharimu sh. bilioni 22.5, baada ya kukamilika kwa ujenzi na ufungaji mitambo, kiwandakitakuwa na uwezo wa kuzalisha mipira ya mikono 20,000 kwa saa sawa na jozi (pairs) 10,000 hivyo kufanya uzalishaji wa jozi 86,400,000 kwa mwaka.
“Hii ni sawa na asilimia 83.4 ya makadirio ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini ya jozi milioni 104 kwa mujibu maoteo ya uhitaji ya bidhaa za gloves nchini mwaka 2023/2024,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, alisema Rais Dkt. Samia amefanya mabadiliko makubwa katika kiwanda hicho na amedhamiria kuona uzalishaji wake unakuwa na tija kwa Watanzania hasa wananchi wa Njombe ambao wameanza kunufaika na fursa zilizopo hususani kupata kipaumbele katika ajira.