Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mpinduzi (CCM), imemteua Paul Makonda kuwa Katibu wa halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi.
Uteuzi huo umefanyika baada ya Halmashauri Kuu ya Chama kukutana jana mjini Dodoma katika kikao chake maalum, chini ya Mwenyekiti Dkt Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana aliyekuwa Katibu Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Sophia Mjema alisema kuwa pamoja na masuala mengine, imeridhia kwa kauli moja na kuielekeza serikali kuendelea na hatua ya utiaji saini mikataba ya uendelezaji na uwekezaji wa bandari.
“Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, imefanya mabadiliko madogo ya Sekretarieti ya halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kwa kumteua Paul Makonda kuwa Katibu wa Halamshauri Kuu CCM Taifa, Itikadi na Uendezi akichukua nafasi ya Sophia Mjema ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa rais Masuala ya Waanwake, Watoto na Makundi Maalum.
Alisema, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imemteua Rabia Abdala Hamid kuwa Katibu wa Halamshauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.
Aidha, Mjema alisema katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imezipongeza Serikali zake zote mbili, Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.