Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imesema katazo la matumizi ya kuni, mkaa linazihusu taasisi zote za umma na binafsi na si kwa mwananchi mmoja mmoja kama inavyotafsiriwa.
Taasisi zote za umma na binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula, kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku zinapaswa kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024.
Zile zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku zinapaswa kusitisha matumizi ya nishati hiyo ifikapo Januari 31, 2025.
Akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo, alisema lengo kudhibiti uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji mkubwa wa miti, kulinda afya za wananchi.
“Bahati mbaya baadhi ya watu walitafsiri lile tangazo tulilotoa Agosti, 2023 hivyo kuwa na wasiwasi itakuwaje kwa mama lishe na majumbani watashindwa kupika, si hivyo, lengo ni kuanza na taasisi zenye watu wengi.
“Ni kweli shule zetu ni watumiaji wakubwa wa kuni, nenda katika taasisi zetu zingine utaona namna gani kuni zinatumika ndio maana tukatoa maagizo haya kwetu sisi wenyewe (taasisi za Serikali na binafsi) tuanze kujipanga katika hili na tutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira,“ alisisitiza Dkt. Jafo.
Aliongeza kuwa, matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo.
Matumizi ya nishati hiyo muda mrefu husababisha magonjwa ya macho.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini mwaka 2019, kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huaribiwa kutokana na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Pia inakadiriwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa kuenea kwa hali ya jangwa, ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia kwa sababu nishati hiyo kupatikana kitahisi, watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.
Kutokana na athari hizo, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda ambapo matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala na kuzalisha majiko sanifu, banifu kwa matumizi ya nishati hiyo.
Jafo alitoa wito kwa kampuni za gesi, mkaa mbadala na majiko banifu zitumie katazo hilo kama fursa ya kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko kwa taasisi hizo.
Itakumbukwa kuwa, Juni Mosi, 2021, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa tamko la Wiki ya Mazingira Duniani na kuzielekeza taasisi, mashirika ya serikali na sekta binafsi zianze kutumia nishati mbadala kupikia, shughuli nyingine za uzalishaji.