Kikwete afurahishwa na uwezo wa wanawake UDSM

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amesema amefurahishwa kuona asilimia ya wahitimu wanawake chuoni hapo imefikia 54.7.

Aliwashauri wanafunzi wanaume kufanye juhudi ili wasiachwe mbali sana na wenzao.

Dkt. Kikwete aliyasema hayo jana kabla ya kuhitimisha Duru la Pili la Mahafali ya 53 ya chuo hicho.

Alisema kwamba, ana kurahi kuona wanawake siku hizi ‘wakiupiga mwingi’ na kuwataka vijana wa kiume walichukulie jambo hilo kama changamoto kwa wao kufanya vizuri zaidi kwenye masomo.

Katika mahafali hayo yalifofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, wahitimu 2796 walihudhuria ambapo 2,700 walitunukiwa Shahada za Awali, kati yao wasichana 1,488 na wavulana 1,212.

Jumla ya Stashahada 78 zilitolewa kwa wanaume 45 na wasichana 33, wakati wanaume 10, wasichana wanane walitunukiwa Astashahada.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye, aliwapongeza wahitimu wote akiwashauri watumie elimu waliyoipata kuleta ushawishi chanya kwa watu wote wanaowazunguka na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.

Prof. Anangisye aliwaasa wahitimu hao kwamba, elimu waliyoipata ni mali ya umma na kwa mantiki hiyo ni lazima ilete faida kwa umma wa Watanzania.

“Elimu haiwezi kuleta faida na kuwa chachu ya mabadiliko yaliyokusudiwa kama haitatumika katika kutatua matatizo ya jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa; “Kama ajira serikalini au katika sekta binafsi zitachelewa kupatikana kuweni wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa, ujuzi wenu unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi,” aliongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *