Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KWA kuwa wanawake na vijana ni msingi, chachu ya mabadiliko katika masuala yote ya kiuchumi na kijamii, serikali imetaka wadau wote kushirikiana ili kuwezesha makundi hayo kuchangamkia fursa zinazoambatana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kundi hilo lina nafasi ya kipekee katika kuelimisha umma kuhusu teknolojia mpya za kidijitali na matumizi salama yenye tija katika TEHAMA.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa wanawake kwenye Kongamano la Saba la Tehama Tanzania.
Kongamano hilo liliandaliwa na Tume ya TEHAMA chini ya uongozi wa Dkt. Nkundwe Mwasaga.
“Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inawashukuru wadau wote wa maendeleo ya TEHAMA kulitambua kundi hili muhimu, kuwawezesha wanawake, vijana ili kuchangamkia fursa zinazoambatana na TEHAMA,” alisema.
Aliongeza kuwa, serikali imeweka mazingira rafiki ya kukuza na kuibua ubunifu, kuchochea uwekezaji na uendelezaji wa Teknolojia za kisasa na TEHEMA kwa kutunga, kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.
Nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide).
Pia nguzo hiyo inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu, mafunzo ya TEHAMA kwa jamii.
Lengo ni kuhakikisha kila mtu bila kujali hali yake au sehemu anayotoka, anashiriki, kufaidika na uchumi wa kidigitali.
“Mtakubaliana nami kuwa, ili maendeleo yaweze kuwa na maana hayana budi kufangamanishwa moja kwa moja na watu,” alifafanua.
Kigezo muhimu cha watu ni kufikiwa kwa makundi yote katika jamii bila ubaguzi wa aina yoyote.
Katika muktadha huo, ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu, matumizi ya TEHAMA kama nyenzo wezeshi hayana budi kufikia makundi yote katika jamii.
Kakele alitoa rai kwa wanawake kutumia jukwaa hilo na fursa hiyo, kupaza sauti zao, kupitia sauti hizo kama taifa tuweze kujadiliana vikwazo vinavyowakabili wanawake na kufanya washindwe kuchangamkia matumizi ya Teknolojia na TEHAMA katika shughuli zao za kila siku.
Alisema katika matumizi hayo, wanawake na vijana wana nafasi maalumu ya kuongoza harakati za kupinga matumizi mabaya ya TEHAMA.
“Sisi kama Wizara yenye dhamana ya TEHEMA nchini, tungependa kusikia sauti zenu, mkielezea fursa zilizopo na changamoto za matumizi ya TEHEMA,” alisema.
Serikali itafurahi kusikia kuhusu mawazo yeo, maoni na matarajio juu ya nini kifanyike ili kujenga mazingira mazuri na rafiki kwa wanawake kufikia na kutumia teknolojia zinazoibukia.
“Wakati tukiendelea kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa TEHAMA nchini, ni vema tukashirikiana kutatua changamoto zinajitokeza kwa wakati. “Tuhakikishe tunatoa elimu kwa umma juu ya matumizi salama ya TEHAMA, kujikinga na matumizi mabaya ya TEHAMA ili kujipatia maendeleo,” alisema.