Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amesema miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, inaiweka Zanzibar katika orodha ya nchi za visiwa zinazoendelea kwa kasi kubwa kiuchumi.
Mbeto aliyasema hayo jana wakati akizindua bonanza la kupongeza miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi, lililoandaliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka, Ussi Haji Gavu akishirikian na Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Kati Unguja.
Alisema maendeleo yaliyofikiwa kwa sasa Zanzibar katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii ni kielelezo cha kujivunia utawala bora unaofuata sheria, utu na haki za binadamu unaosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi.
Alifafanua kuwa, mafanikio yaliyopo katika sekta za elimu, afya, kilimo, maji safi na salama, miundombinu ya usafiri wa anga, majini na nchi kavu, ujenzi wa barabara za kisasa mijini na vijijini vinatakiwa kulindwa, kuthaminiwa ili viwe na manufaa kwa wananchi wote.
“Dhamira ya bonanza hili ni kupongeza miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi, amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo nchini.
“Kila mwananchi ananufaika kwa namna yake, tuendelee kumuunga mkono na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu,” alisema Mbeto.
Katika maelezo yake, Mbeto alisema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Dkt. Mwinyi, tayari Serikali ya Zanzinbar imevuka malengo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2025.
Kupitia bonanza hilo, aliwapongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Mwinyi ambao kasi yao ya kiutendaji inatoa muelekeo wa kupatikana ushindi mkubwa wa dola mwaka 2025.
Bonanza hilo limejumuisha mashindano ya mbio za baiskeli na mbio za Ngalawa ambapo washindi wa walikabidhiwa zawadi mbalimbali.