Kafulila: PPP ni nyenzo kuharakisha maendeleo kwa taifa

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema ubia kati ya Serikali na sekta binafsi ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kafulila ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa uliofanyika jijini Mwanza, uliowakutanisha wakurugenzi, mameneja, wenyeviti wa halmashauri pamoja na wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amesema lengo la ubia wa PPP ni kuiondoa Serikali katika utekelezaji wa majukumu ambayo sekta binafsi inaweza kuyafanya kwa ufanisi na gharama nafuu, hatua itakayosaidia Serikali kuelekeza rasilimali zake katika huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo afya, elimu na uchumi.

Ameeleza kuwa takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha ubora wa rasilimali watu nchini Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika uko katika kiwango cha asilimia 40, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika afya, lishe na elimu bora ili kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki katika uzalishaji na maendeleo.

Akitolea mfano wa Singapore, Kafulila amesema nchi hiyo iliyokuwa na hali inayofanana na baadhi ya nchi za Afrika katika miaka ya 1970, imeweza kuwa miongoni mwa nchi zenye maisha bora duniani, kutokana na uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu, ambao kwa mujibu wa maelezo yake umefikia asilimia 88.

Amesema uzoefu huo unaonesha kuwa maendeleo endelevu yanahitaji uwekezaji katika watu, hivyo kutumia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kutazidi kutaongeza uwezo wa Serikali katika ujenzi wa rasimali watu ambao ni sarafu ya dunia kwa sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *