Maridhiano ya Taifa Yanahitaji Majadiliano Jumuishi

WhatsApp-Image-2026-11-15-at-03.09.11-1024x713 Maridhiano ya Taifa Yanahitaji Majadiliano Jumuishi

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Alexander Makulilo, amesisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu muafaka wa nchi kuwashirikisha Watanzania wa makundi yote ya kijamii, akionya dhidi ya ajenda hiyo kutawaliwa na wanasiasa pekee.

Amesema suala la maridhiano na muafaka wa kitaifa ni pana na linagusa mustakabali wa nchi, hivyo halipaswi kuachwa kuwa jukumu la wanasiasa pekee, bali linahitaji ushiriki wa wasomi, wanazuoni, asasi za kiraia, taasisi za dini, wafanyabiashara, vijana, wanawake na wananchi kwa ujumla.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji huo, Profesa Makulilo amesema uzoefu wa mchakato wa Katiba mpya nchini unaonyesha changamoto zinazoweza kujitokeza pale kundi moja linapochukua nafasi kubwa katika mchakato wa kitaifa na kuyaacha makundi mengine pembezoni.

“Wakati wa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya, kilichokwamisha ni wanasiasa kuhodhi mchakato na kufanya makundi mengine yaonekane kana kwamba hayana nguvu wala nafasi,” amesema.

Amesema wanasiasa wana nafasi muhimu katika majadiliano hayo, lakini wanapaswa kutoa nafasi kwa makundi mengine kushiriki kikamilifu ili ajenda ya muafaka iwe mali ya Watanzania wote na si kundi fulani.

“Wanasiasa wana nafasi yao, lakini makundi mengine yahamasishwe yashiriki kikamilifu katika kujadili muafaka na hatima ya nchi yetu,” amesisitiza.

Profesa Makulilo ameyataja makundi ya kijamii, wasomi, vyama vya wafanyabiashara, taasisi za dini, asasi za kiraia na vyama vya siasa kuwa miongoni mwa wadau wanaopaswa kupewa nafasi katika mchakato huo.

Amesema majadiliano ya kitaifa yanapaswa kuendelea sambamba na juhudi za maridhiano na michakato mingine ya kujenga taifa, akieleza kuwa hatua hizo zinakamilishana katika kurejesha utengamano wa jamii.

“Tunachokitaka ni utengamano wa jamii. Kwa hiyo, tushirikiane kwa pamoja, tuzungumze na kupata muafaka,” amesema.

WhatsApp-Image-2026-11-15-at-03.09.11-1 Maridhiano ya Taifa Yanahitaji Majadiliano Jumuishi
WhatsApp-Image-2026-11-15-at-03.09.11-3 Maridhiano ya Taifa Yanahitaji Majadiliano Jumuishi
WhatsApp-Image-2026-11-15-at-03.09.11-5-1024x682 Maridhiano ya Taifa Yanahitaji Majadiliano Jumuishi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *