Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kutambuliwa kama Malkia wa Nguvu kutokana na hatua kubwa alizochukua katika kuwawezesha wanawake na wasichana, hususan kupitia ujenzi wa shule maalumu za wasichana katika kila mkoa nchini.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa Rais katika kuimarisha elimu na ustawi wa mtoto wa kike, akibainisha kuwa haijawahi kutokea tangu uhuru kwa Serikali kujenga shule maalumu za wasichana katika kila mkoa kwa mpigo.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo usiku wa kuamkia Leo, Novemba 15, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya Tuzo za Malkia wa Nguvu Tanzania 2026 zilizoandaliwa na Clouds Media Group, jijini Dar es Salaam.

“Katika miaka yake minne mpaka mitano iliyopita, Rais amejenga shule maalumu za wasichana kwa kila mkoa, kwa mpigo. Tangu uhuru haikuwahi kutokea hiyo.
“Tumekuwa na shule na hata hizo maalumu tumekuwa nazo, lakini haikuwahi kutokea kujenga shule maalumu kila mkoa kwa ajili ya wasichana, yenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watoto wa kike elfu moja. Hii ni hatua kubwa sana,” amesema.

Amesema juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi zinapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa mwanamke anapopata fursa za kiuchumi, elimu na mitaji, manufaa yake hayaishii kwake pekee bali huenea katika familia na jamii nzima.
Amesisitiza kuwa uwezeshaji wa wanawake unahitaji juhudi za pamoja kutoka serikalini, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kujenga familia imara na jamii yenye maendeleo.
