Tanzania kusisitiza Fedha, teknolojia kupambana na tabianchi COP31

Na Mwandishi Wetu,Uturuki.

TANZANIA imeweka msisitizo katika upatikanaji wa fedha, kujenga uwezo kwa wataalamu na matumizi ya sayansi na teknolojia kama vipaumbele muhimu katika majadiliano ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).

Vipaumbele hivyo vimebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, wakati akiongoza kikao cha viongozi na wataalamu kupitia taarifa ya maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, kilichofanyika jana, Antalya, Uturuki.

1003697541-1024x682 Tanzania kusisitiza Fedha, teknolojia kupambana na tabianchi COP31

Masauni amehimiza ujumbe wa Tanzania kuweka msisitizo katika kuimarisha diplomasia ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi na vipaumbele muhimu vitakavyoongoza majadiliano ya mkutano huo.

Amesema ni muhimu kusisitiza kwa wadau, wabia wa maendeleo na mashirika ya kimataifa umuhimu wa kuiwezesha Tanzania kupata fedha na kujenga uwezo kwa wataalamu wake ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Ni muhimu kusisitiza kwa wadau, wabia wa maendeleo na mashirika ya kimataifa umuhimu wa kuiwezesha Tanzania kupata fedha na kujenga uwezo kwa wataalamu wetu ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Masauni.

1003697540-1024x483 Tanzania kusisitiza Fedha, teknolojia kupambana na tabianchi COP31

Aidha, amesema ujumbe wa Tanzania unapaswa kusisitiza umuhimu wa matumizi ya rasilimali na maliasili za asili zilizopo nchini ili ziweze kutumika vyema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema ujumbe wa Tanzania umejipanga vyema kuhakikisha unapata nafasi ya kutoa sauti yake katika majadiliano hayo na kusisitiza utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa.

“Tumepanga kukutana na wadau na mashirika ya kimataifa ili kuweza kukumbusha ahadi mbalimbali zilizotolewa ikiwemo upatikanaji wa fedha na kusisitiza umuhimu wa kujenga uwezo kwa wataalamu,”amesema Dkt. Muyungi.

Kikao hicho kimefanyika siku ya kwanza ya ufunguzi wa mkutano huo, uliotanguliwa na mkutano wa wataalamu kujadili vipaumbele vya majadiliano ya COP31 mwaka 2026.

1003697539-1024x682 Tanzania kusisitiza Fedha, teknolojia kupambana na tabianchi COP31

Ushiriki wa Tanzania katika COP31 utatoa fursa ya kuitangaza nchi kimataifa kwa kuonesha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kauli mbiu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo inasema: “Hatua jumuishi za Tanzania za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya Dira 2050: Kujenga Taifa Imara, la Kijani na lenye ustawi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *