
Na Mwandishi Wetu, Kenya
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali za Mitaa zina nafasi muhimu katika kuimarisha ushirikiano na kuharakisha mchakato wa ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa jumuiya hiyo katika kuimarisha mifumo ya utawala bora katika Serikali za Mitaa, kubadilishana uzoefu na kuendeleza mipango ya pamoja inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo Novemba 4, 2026, wakati akizungumza katika Jukwaa la Serikali za Mitaa la Afrika Mashariki (EALGF), lililofanyika jijini Nairobi, Kenya, ambapo amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuwa mshirika wa kuaminika katika kuendeleza malengo ya jukwaa hilo na ushirikiano wa kikanda.
Amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano na wizara zote za nchi wanachama wa EAC zinazohusika na Serikali za Mitaa, kwa kushirikiana uzoefu, kujifunza mbinu bora za utendaji na kuunga mkono utekelezaji wa mipango ya pamoja itakayosaidia kuimarisha utawala na huduma za umma.
Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe ameeleza kuwa Tanzania inaunga mkono kuharakishwa kwa utekelezaji wa vipaumbele vya kimkakati vya jukwaa hilo, hususan kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa EACLGA wa mwaka 2026–2031 pamoja na kuandaliwa kwa mkakati endelevu wa upatikanaji wa fedha.
Amesema nyaraka hizo ni muhimu katika kuweka mwelekeo wa taasisi, kuimarisha uhuru wake wa kiutendaji na kuhakikisha inakuwa na rasilimali za kutosha kutekeleza majukumu yake na kuleta matokeo yenye manufaa kwa wananchi wa Afrika Mashariki.
Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza mwenyekiti anayemaliza muda wake kwa uongozi na mchango wake katika kuendeleza jukwaa hilo, huku akimkaribisha mwenyekiti mpya na kumhakikishia ushirikiano kamili wa Tanzania pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI katika kutekeleza majukumu yake.
Amesema dhamira ya Tanzania ni kuona Afrika Mashariki inakuwa jumuiya yenye umoja, ushirikiano na maendeleo endelevu, huku Serikali za Mitaa zikiwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi jumuishi, kuboresha huduma za umma na kuinua maisha ya wananchi.
Jukwaa hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika Mashariki na kufunguliwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora wa Kenya, Dkt. Musalia Mudavadi.










