Sekta binafsi kugharimia 70% ya Mpango wa Maendeleo 2027/28

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

SEKTA binafsi inatarajiwa kugharimia asilimia 70 ya bajeti ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2027/28, kwa kuchangia Shilingi trilioni 62.3 kati ya Shilingi trilioni 89.3 zinazohitajika kutekeleza mpango huo, huku Serikali ikitarajiwa kuchangia Shilingi trilioni 20.7 kupitia bajeti kuu.

Mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yanatarajiwa kuwekeza Shilingi trilioni 6.3, hatua inayoonesha nafasi kubwa ya sekta binafsi katika utekelezaji wa ajenda ya mageuzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akiwasilisha mapendekezo ya mpango huo bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema sekta binafsi inatambuliwa kuwa injini ya mabadiliko ya kiuchumi.

“Sekta binafsi inatambulika kama injini ya mabadiliko ya kiuchumi,” amesema wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge la 13.

Mpango huo ni sehemu ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), unaoweka uwiano wa uchangiaji wa asilimia 70 kwa sekta binafsi na asilimia 30 kwa sekta ya umma, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wawekezaji na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.

Uchumi kulenga ukuaji wa asilimia 6.6Profesa Mkumbo alisema mpango huo unalenga kukuza uchumi kwa asilimia 6.6 mwaka 2027, kutoka asilimia 5.9 mwaka 2025, pamoja na kuzalisha wastani wa ajira mpya milioni 1.7, ikilinganishwa na ajira 981,000 zilizozalishwa mwaka 2025.

Amesema mwaka 2025/26, miradi 934 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 12.5 ilisajiliwa, ikiwa na uwezo wa kuzalisha ajira 307,743.

Aidha, katika robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, miradi mingine 243 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.44 ilisajiliwa, huku sekta ya viwanda ikichukua asilimia 57.2 ya miradi hiyo.

Amesema Serikali imebaini miradi 131 inayoweza kutekelezwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambapo miradi 10 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.Miradi hiyo inajumuisha Kituo cha Biashara Kariakoo, Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).

Amesema Serikali pia inapanga kupunguza vihatarishi vya uwekezaji, kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuharakisha maamuzi ya kibiashara kupitia Mpango Kazi wa Pili wa Kurekebisha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Mazingira ya Uwekezaji (MKUMBI II).

*Kilimo, viwanda na madini kupewa kipaumbele

Akizungumzia sekta zitakazopewa kipaumbele, Profesa Mkumbo amesema kilimo, viwanda na madini vitazingatiwa katika uzalishaji, mauzo ya nje na utoaji wa ajira.

“Maeneo mengine ni uongezaji thamani wa madini, kilimo cha mboga na matunda, ufugaji viumbe maji, uzalishaji wa mafuta ya kula, nguo na mavazi, pamoja na uchakataji wa korosho, sukari na ngano,” amesema.

Katika sekta ya nishati, amesema uwezo wa kuzalisha umeme unatarajiwa kufikia megawati 4,804 ifikapo Juni 2028, kutoka megawati 4,606.14 zilizokuwepo Septemba 2026.

Kwa upande wa usafirishaji, mizigo inayosafirishwa kupitia Reli ya Kati inatarajiwa kufikia tani milioni moja mwaka 2027/28, kutoka tani 810,000 zinazotarajiwa mwaka 2026/27.

Katika sekta za kijamii, Serikali inapanga kuanzisha elimu ya sekondari bila malipo kuanzia mwaka 2028 na kuongeza kiwango cha wananchi wenye bima ya afya hadi asilimia 32.38 mwaka 2027/28, kutoka asilimia 25 ya sasa.

Mpango huo una programu kuu saba, miradi ya kielelezo 38 na maeneo 34 ya mnyororo wa thamani. Taasisi za Serikali zinapaswa kuoanisha mipango yao ya kimkakati na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ifikapo Juni 2027.

*Kamati ya Bajeti yaonya changamoto za utekelezaji

Licha ya malengo hayo, Kamati ya Bunge ya Bajeti imeonya kuwa ongezeko la madeni ya Serikali, ucheleweshaji wa miradi na udhaifu katika matumizi ya fedha za umma vinaweza kukwamisha utekelezaji wa mpango huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki, amesema madeni ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma yaliongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka Shilingi trilioni 3.228 Juni 2022 hadi Shilingi trilioni 6.58 Juni 2025.

Amesema wakandarasi wa barabara walikuwa wanadai Sh trilioni 1.299 mwaka 2025, huku ucheleweshaji wa malipo ukisababisha baadhi yao kusitisha kazi katika maeneo ya miradi.

Kamati pia ilibainisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya umeme wa maji ya Ruhudji na Rumakali, miradi ya chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma, pamoja na mradi wa soda ash wa Engaruka.

Aidha, imeeleza kuwa mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa ulipungua kutoka asilimia 6.8 mwaka 2024 hadi asilimia 5.9 mwaka 2025.

Kutokana na changamoto hizo, kamati ilipendekeza kuboresha upatikanaji wa umeme, kupanua mikopo ya muda mrefu, kuwezesha viwanda vya ndani vya usindikaji na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kilimo.

Mapato ya Serikali yafikia Shilingi trilioni 55.5Katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26, Serikali ilikusanya Shilingi trilioni 55.5 dhidi ya lengo la Shilingi trilioni 56.49, huku matumizi yakifikia Shilingi trilioni 55.6.

Kamati imehimiza udhibiti wa matumizi na usimamizi madhubuti wa fedha za mikopo, ikibainisha kuwa Shilingi bilioni 6.94 zilichepushwa kutoka kwenye miradi mwaka 2024/25.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *