Na Mwandishi Wetu,Mbeya
MIRADI inayotekelezwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) inaendelea kuwa miradi ya Serikali, licha ya jukumu la uendeshaji na ukusanyaji wa mapato kukabidhiwa kwa mwekezaji binafsi kwa mujibu wa makubaliano ya ubia.
Kauli hiyo imetolewa na Innocent Mauki, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, wakati akifungua mkutano wa Market Sounding kuhusu mradi wa PPP jijini Mbeya.

Akifafanua mfumo huo, Mauki alisema utekelezaji wa miradi ya PPP unafanana na Serikali kupata fedha za kugharamia mradi, lakini badala ya Serikali yenyewe kuendesha mradi, kukusanya mapato na kurejesha fedha hizo, jukumu hilo hukabidhiwa kwa mwekezaji binafsi chini ya makubaliano yaliyowekwa.
“Miradi ya PPP ni miradi ya Serikali. Ni sawa na Serikali imekopa, lakini badala ya Serikali yenyewe kukusanya mapato na kulipa mkopo, inamkabidhi mtu mwingine aendeshe mradi,” amesema.

Amesema mkutano wa Market Sounding ni hatua muhimu ya kisheria katika maandalizi ya mradi, inayolenga kukusanya maoni na ushauri wa wadau kabla ya kukamilisha nyaraka zitakazotumika katika mchakato wa kutafuta mwekezaji.
Ameeleza kuwa maandalizi ya mradi yanahitaji nyaraka zinazoeleza kwa kina mradi husika ili kuhakikisha mchakato wa kumtafuta mwekezaji unategemea taarifa na tathmini zilizofanyiwa uhakiki.
Aidha, amesema Serikali hupata msaada wa kifedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya maandalizi ya miradi hiyo, hatua inayowezesha kufanyika kwa tafiti na uchambuzi unaohitajika kabla ya mradi kuingia katika hatua za utekelezaji.
Akizungumzia hatua zinazofuata, Mauki amesisitiza kuwa mkutano huo siyo mchakato wa zabuni, bali ni sehemu ya maandalizi ya mradi, ambapo baada ya hapo mchakato utaendelea katika hatua ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji atakayetekeleza mradi.

Kutokana na umuhimu wa mkutano huo, aliwataka washiriki kutoa maoni yao kwa uwazi na kuzingatia utaalamu wao ili kuboresha maandalizi ya mradi na kuhakikisha masuala mbalimbali yanazingatiwa kabla ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu (Feasibility Study).
Amesema maoni yatakayowasilishwa yatafanyiwa kazi na wataalamu wanaohusika na maandalizi ya mradi, huku tathmini ikiendelea hadi upembuzi yakinifu utakapokamilika na kuweka wazi masuala muhimu ya mradi.