*Watahiniwa 970,876 wamefaulu, ongezeko la asilimia 3.42 ikilinganishwa na mwaka 2025
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuongezeka kwa ufaulu wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026 hadi kufikia asilimia 85.22 kutoka asilimia 81.80 mwaka 2025.
Katika hao waliofaulu, watahiniwa 970,876 wamepata madaraja ya A, B na C.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 3.42, likionesha kuimarika kwa matokeo ya mtihani huo uliofanyika Septemba mwaka huu, ambapo wavulana wameongoza kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 86.18 ikilinganishwa na wasichana waliopata asilimia 84.43.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 3,2026, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 1,168,718 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 637,214 sawa na asilimia 54.52 na wavulana 531,504 sawa na asilimia 45.48.
Amesema kati yao, watahiniwa 1,139,318 sawa na asilimia 97.48 walifanya mtihani, wakiwemo wasichana 624,976 na wavulana 514,342, huku watahiniwa 29,400 sawa na asilimia 2.52 hawakufanya mtihani huo.
Amesema Takwimu zinaonesha kuwa ufaulu wa wasichana umeongezeka kwa asilimia 3.22 kutoka asilimia 81.21 mwaka 2025 hadi asilimia 84.43 mwaka huu, wakati wavulana umeongezeka kwa asilimia 3.67 kutoka asilimia 82.51 hadi asilimia 86.18.

Amesema katika ubora wa ufaulu, watahiniwa 429,667 sawa na asilimia 37.72 wamepata madaraja ya A na B, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.82 ikilinganishwa na mwaka jana.
Kwa upande wa masomo, amesema Kiswahili kimeongoza kwa ufaulu wa asilimia 93.13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.56 ikilinganishwa na mwaka 2025, huku ufaulu wa somo la Uraia na Maadili ukiwa asilimia 90.12.
Ametaja masomo mengine yaliyorekodi ufaulu ni Sayansi na Teknolojia kwa asilimia 80.34, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi asilimia 76.53, Hisabati asilimia 62.56 na English Language asilimia 50.50.
Hata hivyo, amesema licha ya kuongezeka kwa ufaulu katika masomo mbalimbali, Sayansi na Teknolojia imeonesha kushuka kwa asilimia 4.09 kutoka asilimia 84.43 mwaka 2025 hadi asilimia 80.34 mwaka huu.
Aidha, amesema ubora wa ufaulu katika somo hilo kwa watahiniwa waliopata madaraja ya A na B umeshuka hadi asilimia 33.60 kutoka asilimia 48.14 mwaka jana, wakati Hisabati imeonesha kuimarika kwa ubora wa ufaulu kutoka asilimia 21.92 hadi asilimia 32.47.
Katika hatua nyingine, Prof. Mohamed alieleza kuwa Baraza lilizuia kutoa matokeo ya watahiniwa 371 waliougua na kushindwa kufanya mtihani katika idadi kubwa ya masomo au masomo yote, huku wakipewa fursa ya kurudia mtihani huo mwaka 2027 kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani.
Pia, amesema Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 26 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani na wengine watano walioandika lugha ya matusi katika karatasi zao za majibu.
Kuhusu upatikanaji wa matokeo, ameeleza kuwa mwaka huu matokeo yatatolewa bila kuonesha majina ya watahiniwa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ambapo namba za mtihani zitatumika kumtambua kila mtahiniwa.