-Kombo akutana na Mfalme Charles III, viongozi wa Uingereza na Antigua na Barbuda

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imetumia Mkutano wa Viongozi na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) kuimarisha diplomasia ya uchumi na kutafuta fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwamo miundombinu, nishati, kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika mkutano huo uliofanyika Kisiwani Antigua, nchini Antigua na Barbuda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Pembezoni mwa mkutano huo, Balozi Kombo alikutana na Mfalme Charles III wa Uingereza, Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne, pamoja na Gavana Jenerali wa nchi hiyo, Sir Rodney Williams.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa serikali na watendaji wakuu wa kampuni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kujadili namna ya kuongeza uwekezaji, kuimarisha ustahimilivu wa uchumi na kupanua fursa za ajira.
Majadiliano yalijikita katika sekta za miundombinu, nishati jadidifu, kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku msisitizo ukiwekwa katika kuimarisha ushirikiano wa vitendo kati ya serikali na sekta binafsi.
Pia, mkutano huo ulijadili umuhimu wa kuongeza ushiriki wa makampuni na wawekezaji kutoka nchi wanachama ili kukuza biashara, uwekezaji na fursa za kiuchumi.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unalenga kuimarisha mahusiano ya kimataifa, kuvutia mitaji na kukuza ushirikiano wa kiuchumi, sambamba na ajenda ya Serikali ya kukuza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

