Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
DICKSON Msoka(22), anayedaiwa kumuua baba yake mkubwa, Humphrey Elisamon(63), kwa kumjeruhi kwa panga kichwani ameuawa kwa kupigwa na wananchi katika eneo la Mungu Mwema, Hongoro, Kibamba, Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea Oktoba 18,2026 ambapo Dickson, anadaiwa kumuua Humphrey, mkazi wa Hongoro, ambaye ni baba yake mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 19,2026 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amesema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alishambuliwa na wananchi kabla ya polisi kufika eneo la tukio akiwa katika hali mbaya.
Ameeleza kuwa mtuhumiwa alipoteza maisha akiwa anapelekwa hospitalini, huku uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo ukiendelea.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka wananchi kushirikiana na mamlaka mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisheria na kidini kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kuchukua hatua za mkato zenye madhara makubwa,”amesema.
Kamanda Muliro ametoa wito huo wakati Jeshi la Polisi likiendelea na kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kuzungumza na wananchi katika maeneo yao ili kubaini changamoto za uhalifu na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha amewataka Wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kampeni hiyo pindi makamanda wa polisi wanapofika katika maeneo yao.
MWISHO