Tanzania na Saudi Arabia Zasaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Nishati

WhatsApp-Image-2026-10-13-at-03.20.07-1024x768 Tanzania na Saudi Arabia Zasaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Nishati

Riyadh, Saudi Arabia

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kifalme ya Saudi Arabia, zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya nishati, yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo pamoja na kampuni zake za mafuta, gesi na umeme.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Juma Zuberi Homera, na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, pembezoni mwa Kongamano la 25 la Baraza la Petroli Duniani (25th WPC Congress) linalofanyika Riyadh.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Dkt. Homera amesema makubaliano hayo yamefuatia kazi ya wataalamu wa nchi hizo mbili.

Amesema lengo ni kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika sekta ambayo Saudi Arabia imepiga hatua kubwa.

Maeneo yaliyokubaliwa kujadiliwa na kushirikiana ni pamoja na upatikanaji wa bidhaa za mafuta kupitia mikataba ya kibiashara, uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa hizo, na kutathmini fursa zinazotokana na mradi wa gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG).

Pia, nchi hizo zitabadilishana ujuzi na utaalamu katika utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi na kuchunguza fursa za kuanzisha viwanda vya bidhaa zinazotokana na sekta hizo, ikiwamo kemikali za petroli (petrochemicals).

Ushirikiano utahusisha pia umeme na nishati jadidifu, ufanisi wa matumizi ya nishati, teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, nishati safi ya kupikia na biashara ya kaboni.

Maeneo mengine ni matumizi ya akili mnemba na teknolojia za kidijitali katika sekta ya nishati, pamoja na kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wake, Mwanamfalme Abdulaziz amesema makubaliano hayo ni mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano, akisisitiza kuwa urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo unaweza kuimarishwa kupitia kubadilishana utaalamu na kushirikiana katika miradi ya maendeleo ya nishati.

Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhandisi Zena Ahmed Said, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

WhatsApp-Image-2026-10-13-at-03.01.01-1024x646 Tanzania na Saudi Arabia Zasaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Nishati
WhatsApp-Image-2026-10-13-at-03.01.00-1024x559 Tanzania na Saudi Arabia Zasaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Nishati
WhatsApp-Image-2026-10-13-at-03.00.59-1024x768 Tanzania na Saudi Arabia Zasaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Nishati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *