
Na Mwandishi Wetu, Singida
WATU 12 wamefariki dunia, wakiwamo askari watano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida na mahabusu saba baada ya ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Singida-Nzega, eneo la Mlima Sekenke, Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Wengine wawili, ambao ni dereva wa lori la mafuta na mahabusu mmoja, wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale alisema ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 1:30 asubuhi, katika barabara kuu ya Singida-Nzega, eneo la Mlima Sekenke, Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, ikihusisha gari aina ya Lori lenye namba za usajili RAF 243X/TRL 4255 mali ya Kampuni ya YYUSSA ya Kigali Rwanda na Toyota Land Cruiser PT 1982 mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Alisema kuwa Lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Ndanarasa Christian Alfonce, raia wa Rwanda, lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Rwanda lililigonga gari la Jeshi la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Stafu Sajenti (S/SGT) Ussi Hassan likitokea Kituo cha Polisi Shelui kuelekea Kiomboi kupeleka watuhumiwa Mahakamani.
“Waliofariki katika ajali hiyo ni askari watano wa Jeshi la Polisi Tanzania ambao ni SP Frank Lazima Mwasapili ambaye alikuwa ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Shelui, S/SGT Ussi Hassan, SGT Paulo Silivin Gabriel, PC Ashraf Salumu Kheri na PC Nangida Ramadhani Mushi wote walikuwa ni askari wa Kituo cha Polisi Shelui, Singida,”alisema Kamanda Kakwale.
Kamanda huyo aliwataja wengine waliofariki kwenye ajali hiyo ni mahabusu saba ambao ni Timotheo Lazaro Kimaro na Cassian Hassan wakazi wa Doromoni, Fred Musuguli Mazoa, Wilfred Marko Amos na Mariam Hamis Kasijao wote wakazi wa Mingela pamoja na Vivian Saidi mkazi wa Nsusu na Hussen Hussen Kea mkazi wa Tulya.
Aidha kamanda huyo aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Petro Organes Nkana mkazi wa Mingela ambaye ni mahabusu na Ndanarasa Christian Alfonce ambaye ni dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo.
“Majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mandewa, Singida,”alisema.

Aidha, alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alishindwa kumudu gari lake na kuhamia upande wa kulia kisha kuligonga gari la Jeshi la Polisi na kusababisha magari yote mawili kutumbukia korongoni.
Alitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo alama na michoro inayoelekeza jiografia ya barabara husika ili wakuchukue tahadhari na kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na hasara kwa Taifa.