Serikali kuinua zao la Mkonge kwa kununua mashine 10 za usindikaji

IMG-20260806-WA0000-1024x998 Serikali kuinua zao la Mkonge kwa kununua mashine 10 za usindikaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imepanga kununua mashine zaidi ya 10 za kusindika zao la mkonge (dikotiketa maarufu kama Korona) ili kuimarisha usindikaji wa zao hilo kwa wakulima wa ushirika na wale wadogo wanaojitegemea.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa mkonge wenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, huku ikirahisisha upatikanaji wa huduma za usindikaji karibu na maeneo ya uzalishaji.

Akizungumza kwenye Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Simon Kibasa, amesema Serikali imeamua kuwekeza katika mashine hizo kufuatia ongezeko kubwa la wakulima wa mkonge nchini.

Amesema tayari mashine tatu zimenunuliwa na kusimikwa katika maeneo ya Taula (Handeni), Mbuyuni (Mkinga) na Komsala (Handeni), huku nyingine zikitarajiwa kufungwa Makuyuni, Mswaha, Mnazi (Korogwe), Miono (Chalinze), Kishapu (Shinyanga), Kilosa (Morogoro) na Daluni (Mkinga).

Aidha, amesema vituo vya Kibaranga wilayani Muheza na Lucy Estate wilayani Arumeru vimekarabatiwa ili kuongeza uwezo wa usindikaji wa zao hilo.

Kibasa amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji na ubora wa mkonge kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kujiunga na kilimo hicho.

Amebainisha kuwa idadi ya wakulima wa mkonge imeongezeka kutoka wakulima 7,551 mwaka 2019 hadi kufikia zaidi ya 13,000 mwaka 2025, mafanikio ambayo yamechangiwa na kampeni za Serikali za kuhamasisha wakulima, hususan wa Mkoa wa Tanga, kulifanya zao hilo kuwa chanzo kikuu cha mapato.

“Sisi kama Bodi ya Mkonge Tanzania tunaendelea kusimamia ustawi na ukuaji wa zao la mkonge nchini, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira bora ya kuongeza uzalishaji na thamani ya zao hili,” amesisitiza Kibasa.

IMG-20260806-WA0001-1024x1013 Serikali kuinua zao la Mkonge kwa kununua mashine 10 za usindikaji
IMG-20260806-WA0002-1024x1007 Serikali kuinua zao la Mkonge kwa kununua mashine 10 za usindikaji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *